Featured Kitaifa

WAKANGO MSALALA : TUMEACHA MATUSI NA KUCHEZESHA WANAWAKE WAKIWA NUSU UCHI

Written by mzalendoeditor

 
 Mwezeshaji kutoka Mtandao wa Jinsia (TGNP) Aluwa Hamisi Mkilindi akisoma bango la Wakango (Watu waliozaa mapacha) linalosomeka “Mila ya wanawake kucheza wakiwa wamevua nguo haitakiwi”
 
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog Msalala
 
Wacheza Ngoma ya Kimila ya Kabila la Wasukuma (Ukango) kata ya Shilela na Lunguya Halmashauri ya Msalala Mkoani Shinyanga wametangaza kuachana na mila ya kutumia matusi kuwachezesha wanawake wakiwa vifua wazi (nusu uchi) kwani kufanya hivyo ni kudhalilisha wanawake.
 
 
Ukango au Ngoma ya Ukango huchezwa kama watazaliwa Watoto Mapacha( Kurwa na Doto) au Kashinje (mtoto aliyetanguliza miguu). Ngoma hii huchezwa na wanachama maalumu wanaitwa Bhakango na kuna manju maalumu au kiongozi wa watu wanaoifuata mila hiyo.
 
Wakati ngoma hii inachezwa nyimbo zinazoimbwa ni za matusi tu ndiyo hutawala na kama sio mdau huruhusiwi kabisa kusogea na wakati wakicheza ngoma hii wazazi wa watoto Mapacha huwa wako nusu uchi  (vifua wazi) na wamenyolewa vipara na kuvishwa shanga.
 
Ngoma hiyo huanzia nyumbani na kuelekea mtoni au sehemu yoyote yenye bwawa la maji kwa ajili ya kuoga, ambako wote huoga hadharani huku nyimbo za matusi ya nguoni zikiimbwa na maneno mazito ya nguoni yakitamkwa.
 
 
Wakizungumza Novemba 15 & 16, 2022 wakati wa Mkutano wa Tathmini ya kazi zilizofanywa na Vituo vya Taarifa na Maarifa kata ya Shilela na Lunguya na wanajamii kuhusu ukatili wa kijinsia uliokutanisha makundi mbalimbali ya kijamii wakiwemo watu maarufu, waganga wa jadi,Wakango, viongozi wa dini, mila, serikali, sungusungu, vijana na wanafunzi, Wakango wamesema hivi sasa ni marufuku kutumia lugha ya matusi na kucheza ngoma ya Ukango huku wanawake wakiwa vifua wazi.
 
 
Mkutano kuhusu matokeo ya uraghbishi  juu ya masuala ya ukatili wa kijinsia ulijikita katika kujadili hali halisi ya ukatili wa kijinsia kabla na baada ya kuanzishwa kwa Kituo cha Taarifa na Maarifa na namna vituo vya taarifa na maarifa vinavyoshirikiana na jamii na serikali katika kutokomeza matukio ya ukatili wa kijinsia.
 
 
Wakizungumza kwenye mkutano huo, Wakango (watu waliozaa mapacha) akiwemo Mtemi wa Wakango kijiji cha Shilela, Selasini Shitungulu na mmoja wa waliozaa mapacha (mkango) Jumanne Masaga Shitakelelwa wamesema hivi sasa wameachana na mila ya wanawake kucheza ngoma ya ukango wakiwa wamevua nguo (nusu uchi) ambapo wameleeza kuwa  mila hiyo imepitwa na wakati na inadhalilisha wanawake na jamii kwa ujumla.
 
 
“Mara baada ya kupata elimu kutoka kwa Waraghbishi wa wa vituo vya taarifa na maarifa vilivyoundwa na TGNP hivi sasa sisi Wakango tumeachana na mila ya kucheza ngoma ya Ukango wanawake wakiwa vifua wazi lakini pia hatutumii matusi wakati wa ngoma ya ukango”,amesema Shitungulu.
 
“Hizi ngoma za Ukango ambazo tulikuwa tunacheza wakati wa kumtoa mtoto anapozaliwa awe salama kwa sasa zinaonekana haziendani na maadili, hazifai kama ni kutengeneza dawa ili mtoto awe salama siyo lazima wanawake wacheze wakiwa nusu uchi wala kutamka matusi. Tumeona haya mambo ni ya aibu na yanamdhalilisha mwanamke. Ili kulinda utu wa mwanamke tumekataa Kuchezesha wanawake wakiwa vifua wazi na na yeyote anayebainika kukiuka makubaliano yetu tunamlipisha faini ya ng’ombe mmoja au shilingi 40,000/=”,amesema Shitakelelwa.
 
“Zamani ilikuwa kawaida tu kutumia matusi na kuchezesha wanawake wakiwa vifua wazi. Tumebadilika sana baada ya kupewa mafunzo na TGNP kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia,tukapitisha sheria mbalimbali, tunaomba mashirika na taasisi zingine zieneze ujumbe kwenye maeneo mengine kuachana na mila ya kuchezesha wanawake wakiwa vifua wazi na kutoa matusi wakati wa ngoma ya ukango”,ameongeza Katibu wa Mtemi wa Wakango kijiji cha Ndala kata ya Shilela, Philipo John.
 
Naye mwakilishi wa watu maarufu na Sungusungu kutoka kata ya Lunguya, Colnel John amesema wametunga sheria ambapo mtu anayebainika kumpa mimba mtoto anapigwa faini ya ng’ombe mmoja na kwamba hata ngoma za ukango matusi hayatumiki tena kama zamani.
 
Kwa upande wao viongozi wa Jeshi la Jadi Sungusungu (Wasalama) wakiongozwa na Paul Mohamed wameishukuru TGNP kwa kutoa elimu ya masuala ya ukatili wa kijinsia na kwamba elimu hiyo imesaidia kupunguza vitendo vya uhalifu katika jamii ikiwemo kunyanyasa wanawake na kuwapa wanawake haki ya kumiliki mali katika familia.
 
“Sisi Sungusungu tumeshakubaliana kulinda haki za wanawake, hivi sasa mwanaume akiachana na mwanamke lazima wagawane mali, hakuna matukio ya kuua wanaotuhumiwa kuwa ni wachawi, ukioa mwanafunzi tunakupiga sumule (Faini), ukitongoza mwanafunzi tunakupiga sumule ”,amesema Mohamed.
 
“Wanawake msiwe waoga, tunawaalika wanawake kuleta malalamiko ya ukatili mnaofanyiwa myalete Sungusungu  ili tuwashughulikie wanaofanya vitendo vya ukatili”,amesema Mohamed.
 
Nao waganga wa jadi wakiongozwa na Bahati Pius Songa wamesema wameshaachana na ramli chonganishi ambazo baadhi ya waganga walizitumia na kusababisha matukio ya ukatili ikiwemo mauaji ya wanawake wakidaiwa kuwa ni wachawi.
 
“Sasa hivi kama unakuja unaumwa lazima tukuulize kama umeenda pia hospitali, tunaangalia matatizo yako na kukushauri cha kufanya badala ya kukwambia nani kakuroga”,amesema.
 
Afisa Mtendaji wa kijiji cha Ndala kata ya Shilela, Said Pima Katole amekiri kuwepo kwa mabadiliko katika jamii ikiwemo kuwepo kwa usawa katika ugawaji mali za familia, watoto kupelekwa shule, kupungua kwa matukio ya ubakaji na kuwapa mimba wanafunzi huku akihamasisha maeneo mengine kuiga mfano wa Wakango wa kata ya Shilela ambao wameachana na mila ya matusi na kuchezesha wanawake wakiwa uchi.
 

Naye Katibu wa Kituo cha Taarifa na Maarifa kata ya Shilela Meja  Masalu amesema “Kama ilivyo katika kata ya Shilela, Lunguya pia tumeunganisha nguvu na Wakango na Sungusungu hivi sasa wamebadilika na wameweka taratibu za kuachana na lugha za matusi na wamewekeana hadi faini kwa anayebainika anatumia lugha za matusi. Wana Vituo vya taarifa na maarifa tunayo haki ya kujipongeza kwa kubadilisha hili kupitia elimu tuliyotoa”.

Mwezeshaji kutoka Mtandao wa Jinsia (TGNP) Aluwa Hamisi Mkilindi amesema TGNP imekuwa ikishirikiana na Vituo vya Taarifa na maarifa kutoa elimu ya ukatili wa kijinsia katika jamii na wanaendelea kushirikiana kwa pamoja kujenga nguvu ya pamoja (Tapo) katika vuguvugu la kupinga ukatili wa kijinsia huku akihamasisha wananchi kuachana na tabia ya kuficha matukio ya ukatili wa kijinsia.

 

Mwezeshaji kutoka Mtandao wa Jinsia (TGNP) Aluwa Hamisi Mkilindi akizungumza wakati wa Mkutano wa Tathmini ya kazi zilizofanywa na Kituo cha Taarifa na Maarifa kata ya Shilela na Lunguya na wanajamii kuhusu ukatili wa kijinsia Novemba 15,2022. Picha na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Mwezeshaji kutoka Mtandao wa Jinsia (TGNP) Aluwa Hamisi Mkilindi akizungumza wakati wa Mkutano wa Tathmini ya kazi zilizofanywa na Kituo cha Taarifa na Maarifa kata ya Shilela na Lunguya na wanajamii kuhusu ukatili wa kijinsia 
Wanajamii wakiwa na mabango wakati wa Mkutano wa Tathmini ya kazi zilizofanywa na Kituo cha Taarifa na Maarifa kata ya Shilela na Lunguya na wanajamii kuhusu ukatili wa kijinsia
Vijana wakiwa na mabango yanayosomeka “Tujikinge na Machangudoa wakati wa mavuno, Piga kazi siyo Mkeo”
Mabango mbalimbali
Mabango mbalimbali

 

Mratibu wa Vituo vya Taarifa na Maarifa Wilaya ya Kishapu, Fredina Makeleja Said akizungumza kwenye Mkutano kuhusu matokeo ya uraghbishi kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia
Mkango, Jumanne Masaga Shitakelelwa akielezea namna wanavyotokomeza mila na desturi zinazomkandamiza mwanamke na mtoto katika jamii ikiwemo mila ya ukango wanawake kucheza ngoma wakiwa wamevua nguo
Mwakilishi wa viongozi wa Jeshi la Jadi Sungusungu, Paul Mohamed akielezea namna wanavyopambana na ukatili wa kijinsia.
Katibu wa Mtemi wa Wakango kijiji cha Ndala kata ya Shilela, Philipo John akielezea namna walivyoondoa mila ya kutumia matusi na wanawake kucheza ngoma ya ukango wakiwa wamevua nguo.
Mtemi wa Wakango kijiji cha Shilela, Selasini Shitungulu akielezea namna walivyoondoa mila ya kutumia matusi na wanawake kucheza ngoma ya ukango wakiwa wamevua nguo.
Mwakilishi wa kundi la Waganga wa Jadi, Bahati Pius akielezea namna wanavyokabiliana na ukatili wa kijinsia
Afisa Mtendaji wa kijiji cha Ndala kata ya Shilela, Said Pima Katole akielezea namna ukatili wa kijinsia ulivyopungua katika jamii

 

Wanajamii wakiwa kwenye mkutano
Mkutano unaendelea

 

Katekista Kigango cha Ndala kata ya Shilela, Michael Mlekwa akiwasilisha kazi ya kikundi chake wakati wa Mkutano huo
Mwakilishi wa kundi la jamii na watu maarufu, Masanyiwa Kazinza akizungumza kwenye mkutano huo
Mwanafunzi wa shule ya Sekondari Nyikoboko, Othman Mohamed akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari
Wanajamii wakiwa kwenye kazi za vikundi
Wanajamii wakiwa kwenye kazi za vikundi
Wanajamii wakiwa kwenye kazi za vikundi
Wanafunzi wakiwa ukumbini

About the author

mzalendoeditor