Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetia saini Hati za Makubaliano (MoU) 36 wakati wa mkutano wa Biashara na Uwekezaji uliofanyika Dubai leo Februari 26, 2022.
Hati 12 kati ya hizo zimetiwa saini baina ya serikali ya Tanzania kupitia wizara na taasisi za umma na wawekezaji mbalimbali wa sekta za umma na binafsi.
Vile vile, hati za makubaliano nyingine 23 zimetiwa saini baina ya makampuni binafsi kutoka Tanzania na makampuni mengine yenye nia ya kushirikiana katika sekta mbalimbali za kiuchumi.
Hati moja itahusisha Wizara ya Biashara na Viwanda ya Zanzibar na wawekezaji wanaonuia kushirikiana kwenye sekta ya utalii.
Idadi ya ajira zinazotarajiwa kupatikana kwa ujumla kutokana na makubaliano hayo ni zaidi ya 200,000 katika kipindi cha miaka minne, huku uwekezaji huo ukigharimu zaidi ya dola bilioni 7.49 ambayo ni sawa na shilingi trilioni 17.35 za Tanzania.
Sekta zinazotarajiwa kunufaika na hati hizo za makubaliano ni pamoja na nishati, kilimo, utalii, miundombinu, usafiri teknolojia na nyinginezo.
Akiongea katika mkutano huo wa Biashara na Uwekezaji, Rais Samia Suluhu Hassan amesema ili kushawishi uwekezaji na kutengeneza bidhaa madhubuti na za kisasa, nchi inahitaji elimu bora.
“Leo naisihi hasa Serikali ya UAE na nchi nyingine zinazoshiriki kwenye Expo 2020 Dubai kutoa fursa kwa wanafunzi wa Tanzania kusoma kupitia ufadhili na mpango wa ubadilishanaji wa wanafunzi.”