Na Ndahani Lugunya,Kongwa.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe Remedius Mwema Emmanuel amesema kwamba,Viongozi waliokabidhiwa nyadhifa na nafasi mbalimbali katika Jamii hawawezi kupata hekima na busara, endapo kama hawatajiweka karibu na Mwenyezi Mungu.
Alisema hayo wakati akitoa salamu za Serikali ya Wilaya ya Kongwa kwenye Maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50,tangu kuanzishwa kwa Parokia ya Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu-Mlali iliyopo Wilayani Kongwa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma.
Mhe Remidius alisema kwamba Viongozi waliopewa dhamana, mbali na kutoa aridhi kwa ajili ya maendeleo na huduma za Kijamii kama Shule,Zahanati na huduma nyingine za msingi,bado wanao wajibu mkubwa wa kuendelea kutoa ushirikiano kwa Viongozi wa dini ajili ya kazi ya Mungu.
“Baba Askofu kazi ambayo tunaifanya sisi hawa leo ambao wako mbele yako ni waumini wa Kanisa hili lakini wakienda Polisi hawa ni watuhumiwa wakija kwangu mimi ni wananchi.
Kwahio ukiangalia watu ni walewale katika mitizamo tofauti wameendelea kuwa msaada mkubwa na kwa mantiki hiyo imesaidia utekelezaji wa serambalimbali za Serikali na majukumu yetu,” Alisema Mhe Remidius.
Aidha alimshukuru Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma Mhashamu Beatus Michael Kinyaiya na Maparoko wote wanaohudumu katika Parokia mbalimbali zilizopo Wilayani Kongwa,kwa ushirikiano wanaoutoa kwa Serikali katika kusaidia shughuli za kimaendeleo Wilayani humo.
“Ahadi yangu kwako mimi Baba Askofu ni kwamba sisi Viongozi wa Serikali tutaendelea kushirikiana na Kanisa lakini na Viongozi mbalimbali wa kidini kuhakikisha kwamba tunaendelea kuwahudumia watu hawa.
Ukiniuliza kama Mkuu wa Wilaya maeneo ya muhimu ambayo huwezi kuwaondoa wananchi kwenye masuala ya kiimani wananchi ni watiifu sana.kwa hiyo wakati mwingine Serikali unaweza ukatoa maelekezo wananchi wasikuelewe lakini ukimnong’oneza Baba Paroko akazungumza nao wananchi wanaelewa.kwa hiyo tunatambua sana msaada wa Kanisa,” Alisema.
Hata hivyo Mkuu huyo wa Wilaya alitumia fursa hiyo kuwasilisha salamu za Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Kongwa kwa wananchi wote wa Kata ya Mlali.
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma Mhashamu Beatus Michael Kinyaiya,alipongeza Mkuu huyo wa Wilaya kwa kuwa Kiongozi Kijana na kusema kwamba,Vijana wanazo nguvu na hivyo watalitumikia Taifa kwa weredi na utashi mkubwa .
Aidha Askofu Kinyaiya alitumia fursa hiyo kuwaomba waamini na wananchi wote wa Wilaya ya Kongwa kuchukua tahadhari juu ya Maambukizi ya Ugonjwa wa Ebola mapema na si kusubiri hadi utakapoingia ndipo waanze kuchukua tahadhari.
“Naomba kuanzia leo kama hakuna sababu yoyote ya kufanya maandamano tusifanye hivyo na nimetoa mfano kwenu ninyi nyote nimeona Vijana pale getini wakinisubiri sio kwamba sikuwaona lakini nilipita tu makusudi ili baadaye nije kusema hilo.
Kwa hiyo siku nyingine mkisikia nakuja tulieni katika nafasi zenu nitawakuta mpaka nitakapotangaza tofauti.tujikinge mapema kwa sababu akipata mmoja na tukaambukizana hapa itakuwa ni balaa,” Alisema Askofu Kinyaiya.