Kimataifa

SHIRIKA LA POSTA LAPOKEA UGENI WA KAMATI YA MAWASILIANO, ARDHI NA NISHATI YA BARAZA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR

Written by mzalendo

 

Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) Macrice Mbodo akielezea taarifa mbalimbali zinazofanywa na Shirika hilo na namna wanavyoendesha shughuli ili kuwafikia watanzania nchi nzima baada ya kupokea ugeni toka Kamati ya  Mawasiliano, Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar leo Makao Makuu ya Shirika hilo Jijini Dar es salaam.

Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) Macrice Mbodo akikabidhi zawadi ya kalenda na shajara (Diary) kwa 
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Zanzibar Rahma Kassim Ali akiambatana na  Kamati ya  Mawasiliano, Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar leo Makao Makuu ya Shirika hilo Jijini Dar es salaam.

Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) Macrice Mbodo akikabidhi zawadi ya kalenda na shajara (Diary) kwa  Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati,  Yahya Rashid baada akiwa ameambatana na 
  Kamati ya  Mawasiliano, Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar na kutembelea  Makao Makuu ya Shirika hilo Jijini Dar es salaam.

Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) Macrice Mbodo akielezea taarifa mbalimbali zinazofanywa na Shirika hilo na namna wanavyoendesha shughuli ili kuwafikia watanzania nchi nzima baada ya kupokea ugeni toka Kamati ya  Mawasiliano, Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mbodi ameongozana na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Zanzibar Rahma Kassim Ali na  Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati,  Yahya Rashid leo Makao Makuu ya Shirika hilo Jijini Dar es salaam.

 

Wajumbe wa Kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar

 

 

KAMATI ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar leo tarehe 21 Januari imelitembelea Shirika la Posta Tanzania (TPC) ili kujionea utendaji na huduma mbalimbali zinazotolewa na Shirika hilo.
Kamati hiyo ilianza ziara hiyo kwa kupokea kupokea taarifa ya utendaji ya Shirika hilo ikiangazia historia ya kuanzishwa kwake, mapito mbalimbali lililopitia Shirika tangu kuazishwa kwake mwaka 1994 hadi sasa. Pia mwelekeo wa sasa wa Shirika katika kutoa huduma zake.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Bwana Yahya Rashid amesema wamefurahishwa na utendaji kazi wa Shirika la Posta Tanzania hususan ni namna lilivyojipanga kwenye kuhakikisha wananchi wanapata huduma zenye tija kulingana na mahitaji yao ya sasa.  
Aidha, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Yahya Rashid amelipongeza Shirika la Posta nchini kwa kuendelea kukuza na kuimarisha uhusiano kati yake na Taasisi mbalimbali zilizopo visiwani Zanzibar kwani ushirikiano huo utaboresha zaidi upatikani wa huduma mbalimbali kwa pande zote za Muungano wa Tanzania.  
“Napongeza ushirikiano uliopo kati ya Serikali zetu za Tanzania Bara na Zanzibar kupitia Taasisi zetu hizi kwani kutaleta huduma bora kwa wananchi wetu”. Alisema Yahya
Katika hatua nyingine, Yahya amelitaka Shirika la Posta kuhakikisha linatoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi sahihi ya huduma za Posta nchini kwani wananchi wanapaswa kufahamu na kutumia huduma za Posta za kisasa za kidijitali.
“Wananchi wanahitaji kuelimishwa kuhusu huduma za Posta, mkawajengee uelewa wa kutosha kwa sababu Shirika la Posta lina fursa za kibiashara na  kuna huduma za kidigitali na gharama zake ni nafuu na ni za uhakika”. Amesema Yahya.
Kwa upande wa Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Rahma Kassim Ali aliyeambatana na msafara wa Kamati hiyo amesema kufika kwao kama Wizara katika  Shirika la Posta kumesaidia kufahamu masuala mbalimbali ambapo hawakuwa na uelewa nayo na kupata elimu na ufahamu wa mambo mengi ya msingi na yenye manufaa kwa jamii ya watanzania.
“Nimefarijika sana kufika hapa leo, nimepata nafasi ya kujifunza na kufahamu namna Shirika la Posta linavyofanya kazi zake kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar, hii itatusaidia sana kwenye mambo mengi tunaosimamia sekta ya mawasiliano”. Amesema Rahma.
Aidha,  Waziri ameahidi kuwa, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara yake itaendelea kutoa ushirikiano kwa Shirika la Posta nchini ili kuhakikisha wananchi wa pande zote za Muungano wanapata huduma bora na zenye tija kwa manufaa ya Taifa kwa ujumla.
Naye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye ameishukuru na kuipongeza Serikali ya Zanzibar kupitia Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kwa kuona umuhimu wa kufika Makao Makuu ya Shirika la Posta nchini na kujionea shughuli mbalimbali pamoja na huduma zinazotolewa na Shirika hilo. Pia ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika kuhakikisha wananchi wa pande zote za Muungano wananufaika na huduma za Posta.
 Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Macrice Mbodo ameishukuru Kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati kwa kutenga muda wao na kuja kulitembelea Shirika la Posta . Kaimu Postamasta Mkuu ameongeza kuwa, zipo fursa mbalimbali ambazo Shirika la Posta linazifanyia kazi kwa upande wa Zanzibar ikiwemo Duka Mtandao ambalo linawawezesha wananchi kuuza na kununua bidhaa zao katika duka hilo na kufikishwa popote walipo. Pia fursa ya huduma za usafirishaji ambapo mwananchi ataweza kufikishiwa bidhaa na huduma mahali popote alipo kupitia mfumo wa anuani za Makazi na Postikodi unaoendelea kujengwa hapa nchini kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Katika hatua nyingine, Kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar pamoja na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Rahma Kassim Ali walipata wasaa ya kutembelea Kituo cha Huduma Pamoja kinachotoa huduma mbalimbali za kiserikali, kilichopo katika Ofisi kuu ya Mkoa wa Dar es Salaam na kujionea huduma mbalimbali zinazotolewa katika kituo hicho.

 

About the author

mzalendo