Featured Kitaifa

MAADHIMISHO YA SIKU YA KIMATAIFA YA MTOTO WA KIKE 

Written by mzalendoeditor

Tarehe 11 Oktoba ya kila mwaka Tanzania uungana na nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Mataifa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike ambapo lengo la maadhimisho ni kutoa fursa kwa wadau wanaotekeleza afua za watoto hususani watoto wa kike kufanya tathmini ya upatikanaji wa haki, ulinzi na maendeleo ya watoto kwa ujumla na kupendekeza hatua stahiki katika kuboresha huduma hizo. 

Kwa Mwaka huu 2022, Kaulimbiu inayoongoza Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike ni; “Haki Zetu ni Hatima Yetu; Wakati ni Sasa”. Kaulimbiu hii inahimiza utoaji wa haki sawa kwa Watoto wote bila ubaguzi katika familia na kwenye jamii yetu. Katika miaka 10 ya utekelezaji wa haki za watoto, umakini umeongezeka katika kuainisha na kusimamia upatikanaji wa haki kwa watoto wote huku mkazo zaidi ukiwekwa kwa watoto wa kike. Pamoja na jitihada hizo, bado watoto wa kike wanaendelea kukabiliwa na changamoto nyingi zinazohusu usalama wao ikiwa pamoja na kubakwa na mimba za mapema hivyo kukatiza ndoto zao. 

Katika kuhakikisha utekelezaji wa afua zinazohusu haki na ustawi na maendeleo ya mtoto zinatekelezwa kwa ufanisi Serikali imeendelea kuboresha huduma za malezi ya watoto wakiwemo wasichana kwa kutoa mafunzo ya malezi chanya kwa wazazi na walezi kwa lengo la kuwezesha makuzi bora ya watoto katika Halmshauri 132 ambapo vikundi vya malezi 1,184 vilianzishwa katika Mikoa 17 ya Tanzania Bara hadi kufikia Juni 2022.

Vikundi hivyo vimetoa mchango mkubwa katika kuhamasisha jamii kuachana na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto, kuchangia nguvukazi katika ujenzi wa vituo vya kijamii vya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto na kuimarisha nidhamu ya wazazi na watoto kwa kuendelea kutoa elimu hiyo katika ngazi ya jamii.

Katika nchi yetu maadhimisho haya yatafanyika katika ngazi ya Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na yatafanyika kulingana na mazingira ya Mkoa na Halmashauri husika. Ni muhimu kwa kila Mkoa kufanya maadhimisho haya ili kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kutoa haki kwa kuzingatia usawa wa kijinsia kwa watoto wote. 

Wizara itashirikiana na Mkoa wa Mara katika kilele cha maadhimisho haya kitakachofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti. Aidha, Wizara itashirikiana na Mkoa wa Manyara katika kufanya kampeni ya kutokomeza ukatili dhidi ya watoto hususani ukeketaji katika Wilaya zote za Mkoa huo ambapo kilele cha kampeni hizo itakuwa tarehe 12 Oktoba, 2022 katika Halmashauri ya Mji wa Babati. 

Mwisho, natoa rai kwa wananchi wote kuhamasishana kuhusu Haki, Ulinzi, Ustawi na Maendeleo ya Watoto hasa watoto wa kike ambao ndio wahanga wakubwa katika familia na Jamii. Niwaombe wananchi kujitokeza kwa wingi katika Mikoa na Halmashauri zetu kushiriki kwenye Maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike. 

About the author

mzalendoeditor