Featured Kitaifa

MAKAMU WA KWANZA WA RAIS ZANZIBAR AFUNGUA KONGAMANO LA BIASHARA KATI YA TANZANIA NA ITALIA

Written by mzalendoeditor

Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman akifungua
rasmi Kongamano la Pili la Uwekezajikati ya Tanzania na Italia
lililofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip Zanzibar tarehe 28 Septemba,
2022. Pamoja na mambo mengine, Mhe. Othman ametoa wito kwa wawekezaji
kutoka Italia na duniani kote kuwekeza Tanzania katika fursa mbalimbali
za manufaa.

…………………………….

Makamu wa Kwanza wa Rais wa
Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman amesema Serikali ya Zanzibar inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuwawezesha Wawekezaji wenye tija  kuwekeza katika sekta
mbalimbali  ikiwemo sekta ya Uchumi wa Bluu.

Mhe. Othman ametoa kauli hiyo wakati akifungua rasmi Kongamano la Pili la
Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika Zanzibar tarehe
28 Septemba, 2022 na kuwashirikisha wadau mbalimbali wa masuala ya biashara na
uwekezaji kutoka Tanzania na Italia.

Mhe. Othman ambaye alimwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwenye kongamano hilo amesema Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar imefungua milango kwa wawekezaji wenye nia ya kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali na kwamba inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara
kwa kuzifanyia maboresho sheria na kanuni mbalimbali za uwekezaji.

 

Kadhalika alisema maboresho
hayo yanakwenda sambamba na yale ya sekta ya utoaji huduma kama vile za viza,
vibali vya kazi na ukaazi pamoja na  kuboresha
mawasiliano kupitia mifumo ya kidigitali ambapo Serikali hiyo inatarajia hivi
karibuni kuzindua  mfumo wa uombaji viza kwa njia ya mtandao.

“Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea kuboresha mazingira ya
uwekezaji ili  kuifanya Zanzibar kuwa miongoni mwa
maeneo bora ya uwekezaji duniani
. Uwekezaji una manufaa
makubwa ya kiuchumi kwa nchi ikiwa ni pamoja na kukuza pato la taifa pamoja na  kutenegeneza ajira kwa vijana na wanawake
” alisema Mhe. Othman.

Mhe. Othman ameeleza kuwa, katika kipindi cha miaka miwili kuanzia mwezi
Novemba 2020 hadi wakati wa kongamano hilo Zanzibar imesajili miradi ya uwekezaji
196 yenye thamani ya dola za marekani bilioni 1. 4 ambapo miradi hiyo inatarajiwa
kutengeneza ajira zipatazo 9,000. Hivyo alihimiza
washiriki kutumia  Kongamano hilo kama  chachu ya kuhamasisha wawekezaji wengi zaidi
kuja nchini.

 

“Kongamano hili liwe chachu
ya kuvutia na kuhamasisha wawekezaji zaidi kuja Zanzibar na Tanzania kwa
ujumla. Naendelea kutoa wito kwa wawekezaji kutoka Italia na duniani kote
kuchangamkia fursa lukuki za uwekezaji tulizonazo. Namaliza kwa kusema Wekeza
Zanzibar, Wekeza sasa” alisisitiza Mhe. Othman

Awali akizungumza wakati wa kongamano hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mhe. Mudrick Soraga amepongeza jitihada zinazofanywa
na Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo na Balozi
mwenzake wa Italia hapa nchini, Mhe. Marco Lombardi za kuandaa kongamano hilo
kwa mara ya pili ikiwa ni mchango wao wa  kuhakikisha nchi hizi mbili zinanufaika
kupitia ushirikiano mzuri uliopo.

 

Pia aliwataka washiriki wote
kutumia kongamano hilo kama fursa ya kubadilishana  mawazo na uzoefu miongoni mwao ili kuendelea
kuboresha sekta ya biashara na uwekezaji  nchini. 

 

 Mhe. Soraga  pia alitumia fursa hiyo kuainisha fursa za
kipaumbele za uwekezaji Zanzibar kuwa ni pamoja na Sekta ya Uchumi wa  Bluu, Kilimo, Usindikaji wa mazao ya kilimo,
Utalii, ufugaji wa samaki, utalii unaozingatia
utunzaji wa mazingira , miundombinu, nishati na uwekezaji katika mali
zisizohamishika kama majengo.

 

Wakati wa Kongamano hilo
mada mbalimbali ziliwasilishwa na kujadiliwa ikiwemo Maendeleo ya Miundombinu,
Uchumi wa Bluu na Kilimobiashara na Kilimo cha Kisasa cha kutumia mashine na
mitambo. Kongamano hilo ambalo limewashrikisha wadau kutoka sekta mbalimbali za
biashara na uwekezaji wa hapa nchini na kutoka Italia litahitimishwa rasmi
tarehe 30 Septemba 2022 jijini Dar es Salaam.

 

Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman akifungua
rasmi Kongamano la Pili la Uwekezajikati ya Tanzania na Italia
lililofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip Zanzibar tarehe 28 Septemba,
2022. Pamoja na mambo mengine, Mhe. Othman ametoa wito kwa wawekezaji
kutoka Italia na duniani kote kuwekeza Tanzania katika fursa mbalimbali
za manufaa
Sehemu ya Washiriki wa Kongamano wakifuatilia hotuba ya ufunguzi kutoka kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mhe. Mudrick Soraga nae akizungumza wakati wa Kongamano hilo
Sehemu ya Mabalozi na wageni waalikwa wakifuatilia hotuba ya Mhe Soraga
Mkurugezni Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) akifafanunua fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo Zanzibar
Mhe. Makamu wa Kwanza wa Rais akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (kushoto) na Balozi wa Italia nchini, Mhe. Marco Lombardi (katikati)
Sehemu ya washiriki wa kongamano
Sehemu nyingine ya washiriki
Mhe. Balozi Lombardi akizungumza na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Ofisi ya Mambo ya Nje Zanzibar, Bi.  Leluu Abdallah (kushoto) na Afisa Mambo ya Nje, Bi. Salma Baraka     

 

 

About the author

mzalendoeditor