Featured Michezo

WAZIRI BASHUNGWA ATOA MAAGIZO MAZITO KWA MIKOA, HALMASHAURI

Written by mzalendoeditor

Na Shamimu Nyaki

Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Innocent Bashungwa ametoa maelekezo kwa Mikoa na Halmashauri zote nchini, kutenga fedha kwa ajili ya kujenga na kukarabati miundombinu ya michezo nchini.

Mhe. Bashungwa ametoa maelekezo hayo leo Septemba 16, 2022 Bungeni jijini Dodoma, wakati akitoa majibu ya nyongeza katika maswali ya Waheshimiwa Wabunge kuhusu Serikali kujenga miundombinu na viwanja vya michezo.

“Ofisi ya Rais TAMISEMI inashirikiana kwa karibu sana na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo katika kuendeleza sekta ya michezo ngazi ya Halmashauri, nasisitiza maeneo yote ya michezo katika shule zote za Msingi na Sekondari kupimwa na kutambua maeneo ya michezo na kuyalinda ili yasivamiwe” amesisitiza Mhe. Bashungwa.

Aidha, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul akijibu swali la  nyongeza la Mhe. Sophia Mwakagenda kuhusu ujenzi wa miundombinu ya mchezo wa Masubwi, amesema uwekezaji unaosisitizwa unajumlisha pia miundombinu ya mchezo huo.

Katika hatua nyingine, Naibu Spika wa Bunge Mhe. Mussa Azan Zungu  ametoa Pongezi kwa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo  ikiongozwa na Waziri Mhe. Mohamed Mchengerwa, Naibu Waziri Pauline  Gekul,  Katibu Mkuu Dkt.Hassan Abbasi  na Naibu Katibu Mkuu Saidi Yakubu kwa mapinduzi waliyofanya katika wizara hiyo.

About the author

mzalendoeditor