Featured Kitaifa

WACHANGIA DAMU MARA KWA MARA SASA KUTAMBULIKA KWA KADI ZA KIELETRONIKI

Written by mzalendoeditor

Na. WAF – Dar Es Salaam

Serikali kupitia wizara ya Afya imejipanga kutoa kadi za kieletroniki kwa wachangiaji damu wanaojitolea mara kwa mara angalau mara tatu kwa mwaka.

Hayo yamesemwa leo Februari 25, 2022 na Waziri wa afya Mhe. Ummy Mwalimu alipokuwa katika ziara ya kutembelea makao makuu ya mpango wa Taifa wa damu salama jijini Dar es Salaam.

Waziri Ummy amesema Kadi za kieletroniki zitaepusha usumbufu kwa wachangia damu endapo watahitaji huduma ya damu kwani kadi hizo zitaonesha jina la mchangiaji damu, kundi la damu yake na namba ya kadi, na mchangiaji huyu atapewa kipaumbele akiwa na mgonjwa hata yeye mwenyewe.

“Kila Mtanzania ana haki ya kupata damu lakini kwa wale ambao watakaokuwa na kadi watapewa kipaumbele cha kwanza”. Amesema Waziri Ummy.

Katika hatua nyingine Waziri Ummy amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeamua kutoa bure mifuko ya kukusanyia damu salama pamoja na vifaa vya ukusanyaji kwa Halmashauri zote nchini 184 ili kwenda kumaliza changamoto ya ukusanyaji ambayo imejitokeza nchini hivi sasa na kusababisha uhaba wa damu katika vituo vya kutolea huduma za afya.

“Nitoe wito kwa waganga wakuu wa mikoa yote nchini kuhakikisha wanapokea vifaa hivyo vya kuchangia damu na kuwahamasisha wananchi kujitokeza kuchangia damu ili kutatua changamoto ya upatikanaji damu kwa kuwa damu inahitajika sana na mama wajawazito, watoto, watu waliopata ajali pamoja na wanaofanyiwa upasuaji”. Amesema Waziri Ummy.

Kwa upande wake Mganga mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Rashid Mfaume amesema vifo vingi vya kina mama wajawazito hutokana na ukosefu wa damu salama na hivyo kuitaka jamii iweze kujitokeza kuchangia damu ili kuokoa maisha kwa wenye uhitaji huku akieleza kuhamasisha vikundi mbalimbali kujitokeza kwa ajili ya uchangiaji.

Naye, Meneja mpango wa Taifa damu salama Dkt. Magdalena Lyimo ameishukuru Serikali kwa hatua inayochukua juu ya upatikanaji damu salama kwa urahisi.

“Sasa kazi ni kwetu kuhakikisha damu salama inapatikana kwa kuungana na wananchi juu ya uchangiaji damu na naamini tukishirikiana tutaokoa vifo vingi”. Amesema Dkt. Lyimo.

About the author

mzalendoeditor