Featured Kimataifa

MAJESHI YA URUSI YAINGIA MJI MKU WA UKRAINE, KIEV

Written by mzalendoeditor
Milio ya risasi na makombora imesikika katika Mji Mkuu wa Ukraine, Kiev huku vifaru vya kivita vyenye bendera za Urusi vikionekana kwa mara ya kwanza nje kidogo ya Kiev, ikiwa ni ishara kwamba majeshi ya Urusi tayari yameshaingia.

Kwa mujibu wa mashuhuda, milio ya risasi na makombora imerindima usiku kucha nje kidogo ya Kyiv wakati majeshi ya Ukraine yakipambana na majeshi ya Urusi yanayozidi kusonga mbele kutokea pande tatu, Mashariki, Kaskazini na Kusini mwa nchi hiyo.
Waziri wa Ulinzi wa Ukraine, amekaririwa akiwaambia wakazi wa maeneo ambayo vifaru vya Urusi vimeonekana ikiwemo kitongoji maarufu cha Obolon, kuvichoma moto na kutumia mabomu yanayotengenezwa kienyeji maarufu kama Molotov Cocktails ili kuilinda nchi yao dhidi ya uvamizi.
Wakati hayo yakiendelea, serikali ya Ukraine imetangaza kuwa ni marufuku kwa wnaume wenye umri wa kuanzia miaka 18 hadi 60 kuondoka ndani ya nchi hiyo na kuwataka kubaki ili kupambana na uvamizi wa Urusi, huku Rais… akiagiza raia wote wanaotaka silaha za kivita, wapewe ili kuilinda nchi hiyo.
Wanawake, watoto na wazee ndiyo pekee wanaoruhusiwa kwenda katika maeneo salama au kutoka ndani ya mipaka ya nchi hiyo kwa ajili ya kutafuta hifadhi ya ukimbizi katika nchi jirani.
Taarifa kutoka Shirika la Habari la Reuters, zinaeleza kuwa chanzo kimoja ndani ya Wizara ya Ulinzi ya Urusi, kimeeleza kuwa ndege ya kivita ya Ukraine imetunguliwa na majeshi ya Urusi jijini Kyiv huku wizara ya Ulinzi ya Ukraine ikidai kwamba ndege iliyotunguliwa ni ya Jeshi la Urusi.
Makabiliano ya vikosi vya ardhini kati ya majeshi ya nchi hizo mbili, yameendelea kupamba moto ambapo inaelezwa kwamba wanajeshi wa Ukraine wamekuwa wakilipua madaraja, kama njia ya kuyazuia majeshi ya Urusi kuingia ndani ya Jiji la Kyiv.
Wakati hayo yakiendelea, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov amesema serikali ya Moscow ipo tayari kwa mazungumzo na Ukraine lakini kwa sharti kwamba wanajeshi wa Ukraine wanapaswa kuweka silaha chini na kusalimu amri.

About the author

mzalendoeditor