Featured Kitaifa

NAIBU WAZIRI SAGINI ATOA MUDA WA UKOMO WA HIARI WA UKAGUZI WA MAGARI

Written by mzalendoeditor

NAIBU Waziri Sagini ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani akisalimiana na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani,SACP Wilbroad Mutafungwa leo, alipowasili Bwalo la Maofisa wa Polisi Oysterbay kuzungumza na Wajumbe wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani.

NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Sagini ambae pia Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani akiongoza Kikao cha Baraza la Taifa la Usalama Barabarani kilichofanyika Ukumbi wa Maofisa wa Polisi Oysterbay, Dar es Salaam. Kushoto ni Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, SACP Wilbroad Mutafungwa.

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, SACP Wilbroad Mutafungwa ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Usalama Barabarani akizungumza na Wajumbe wa Baraza waliohudhuria leo katika kikao cha Baraza hilo, Ukumbi wa Maofisa wa Polisi Oysterbay, Dar es Salaam.

WASHIRIKI wakifatilia Kikao cha Baraza la Taifa la Usalama Barabarani kilichofanyika Ukumbi wa Maofisa wa Polisi Oysterbay, Dar es Salaam. Kushoto ni Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, SACP Wilbroad Mutafungwa.

………………………………………………

Na Mwandishi wetu, MoHA

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Usalama Barabarani Jumanne Sagini ameweka muda wa ukomo wa ukaguzi wa magari kwa hiari kwa wamiliki na madereva wa vyombo vya moto pamoja na ukaguzi unaoambatana na utoaji wa stika za usalama barabarani baada ya magari hayo kukaguliwa na Wakaguzi kutoka Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani.

Akizungumza Jijini Dar es salaam leo katika Bwalo la Maofisa la Oysterbay, Naibu Waziri Sagini, alisema kuwa, zoezi la ukaguzi wa magari kwa hiari lilianza rasmi Novemba 23, 2021 baada ya Uzinduzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani yaliyofanyika Kitaifa mkoani Arusha uliozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan .

Aidha, Naibu Waziri Sagini amewaeleza wamiliki wa vyombo vya moto kuwa, baada ya Marchi 30, 2022 chombo chochote cha moto kitatakiwa kuwa na stika ya usalama barabarani baada ya chombo hicho kufanyiwa ukaguzi na kupewa stika na kwamba chombo cha moto kitakachoshindwa kufanya hivyo kitachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kutozwa faini ya kushindwa kufanyiwa ukaguzi wa hiari sambamba na chombo hicho kupelekwa kwenda kufanyiwa ukaguzi wa lazima.

“Chombo chochote cha moto kitakachotumika barabarani kinatakiwa kiwe na stika ya usalama barabarani baada ya chombo hicho kufanyiwa ukaguzi na kupewa stika hiyo. Vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa.” Alisema.

Aidha, Baraza la Taifa la Usalama Barabarani linapenda kuwapongeza baadhi ya wamiliki na madereva wa magari kwa ushirikiano mkubwa wanaoendelea kutoa katika usimamizi wa usalama barabarani na pia kutoa onyo kali kwa wamiliki na madereva wa magari wanaotumia magari yao barabarani na kusababisha ajali kwa kuendesha mwendo kasi na kuyaingiza barabarani yakiwa mabovu na kusababisha ajali.

About the author

mzalendoeditor