Featured Kitaifa

DITOPILE AMPONGEZA RAIS SAMIA KWA KUTOA MBOLEA YA RUZUKU

Written by mzalendoeditor

MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma ambaye pia ni Mkulima, Mariam Ditopile amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa mageuzi makubwa aliyoyafanya katika sekta ya Kilimo ambapo kwa mara ya kwanza bajeti ya Uzalishaji wa Mbegu imeongezeka kutoka Sh Bilioni 10.5 hadi Sh Bilioni 43.03.

Hayo ameyasema jijini Dodoma katika mkutano wake na wandishi wa habari ambapo amesema kwa kipindi kifupi cha Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan mageuzi makubwa yamefanyika katika sekta ya Kilimo kulinganisha na miaka ya nyuma ambapo kilio kikubwa kilikuepo.

Amesema Rais Samia ndani ya muda mfupi amewezesha kupatikana kwa bajeti bora ya Kilimo ambapo kwa mwaka huu wa fedha 2022/23 Wizara ya Kilimo imetengewa Sh Bilioni 751 huku Sh Bilioni 631 zikielekezwa kwenye miradi ya maendeleo.

Mbunge Ditopile ameongeza kuwa ongezeko la Bajeti ya Kilimo kwa mwaka huu wa fedha ni takribani asilimia 300 kulinganisha na bajeti ya mwaka 2020/21 ambapo kiasi kilichotengwa ni Sh Bilioni 229 na kati ya fedha hizo ni Sh Bilioni 150 pekee ndio zilienda kwenye miradi ya maendeleo.

” Rais Samia pia amejidhatiti kwenye eneo la tafiti za Kilimo, Bajeti ya tafiti za Kilimo imepanda kutoka Sh Bilioni 7.3 kwa mwaka 2020/21 hadi Sh Bilioni 40 kwa mwaka huu wa fedha. Tunamshukuru Rais pia kwa kupandisha bajeti ya Uzalishaji mbegu kutoka Sh Bilioni 5.4 hadi Sh Bilioni 43 kwa mwaka huu wa fedha 2022/23.

Pia tumeshuhudia utaratibu mzuri wa kuwawezesha wakulima nchini kupata Mbegu za Alizeti ambapo gharama zote ni Sh 3,500 tofauti na bei ambayo haikua na ruzuku ambayo ilikua ni kSh 7,000 hadi 8,000,” Amesema Mbunge Ditopile.

Amesema kwa namna ambavyo Rais Samia ameonesha mageuzi makubwa kwenye sekta ya Kilimo wao kama Wakulima wanampongeza Rais Samia kwa jitihada za dhati za kuwakomboa Wakulima kwani ni wazi mchango wa mbolea ni mkubwa katika sekta ya Kilimo hususani katika kuongeza tija.

” Tunamshukuru Rais Samia na Serikali yake kwa usikivu wao kwetu sisi Wakulima kwa kutuletea mfumo mzuri wa Mbolea ya Ruzuku pamoja na kutoa kipaumbele kwa wazalishaji wa ndani ili kulinda viwanda vyetu, ajira na Usalama wa chakula.

Katika hili Serikali ya awamu ya sita imefanya kazi kubwa ya kuvutia wawekezaji ambapo sasa tunashuhudia ujenzi mkubwa wa kiwanda cha Mbolea cha Intracom Fertilizer kinachojengwa jijini Dodoma na mwekezaji kutoka Burundi, uwekezaji wa kiwanda hiki utatoa ajira zaidi ya 3000 kwa watanzania,” Amesema Ditopile.

About the author

mzalendoeditor