NJOMBE
Mwanafunzi wa darasa la sita Marko Sanga (12) amekutwa amejinyonga kwa kutumia mnyororo wa Baiskeli katika Kijiji cha Maleutsi wilayani Makete mkoani Njombe kwa kile kinachodaiwa kuwa kutokana na radio, nguo za shule pamoja na madaftari kuungua kwa shoti ya umeme.
Kwa mujibu wa mama yake mkubwa na marehemu huyo Obina Mbilinyi amesema kuwa mtoto huyo walikuwanaye shambani na jioni ilipofika walimwambia atangulie nyumbani ili akafungue ng’ombe malishoni na kuwarudisha nyumbani ambapo alipofika nyumbani alikuta vitu hivyo vimeungua kwa shoti ya umeme iliyosabishwa na radio ambayo marehemu alikuwa ameichomeka kwenye umeme.
Amesema marehemu alifungua ng’ombe kama alivyoagizwa na kisha kujinyonga na ndipo tuliporudi nyumbani tulimtafuta na kumkuta akiwa amekufa huku akining’inia kwenye mnyororo wa baiskeli.
“Tunahisi kuungua kwa radio na baadhi ya vitu vyake inaweza kuwa ni sababu ya kujinyonga kwake maana mpaka tunaagana shambani alikuwa katika hali ya kawaida”.
Aidha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe Hamis Issah amethibisha kutokea kwa tukio hilo na kuwataka wazazi kuishi vizuri na watoto wao kwani inawezekana mtoto huyo alikuwa anahofia kuadhibiwa kwa kile kilichotokea ndipo akaona ni heri kufa.
“Wazazi kuweni makini na watoto msipende kuwaadhibu kila wanapokosea kwani watoto wa siku hizi ni kama yai, ukiwa unamuadhibu mara kwa mara matokeo yake huwa kama haya maana wanajawa na hofu”.