Featured Kitaifa

WAZIRI NAPE AHAMASISHA WANANCHI KUTOA USHIRIKIANO KWA MAKARANI WA SENSA

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (kushoto), akizungumza katika kipindi cha Morning Trumpet cha Televisheni ya Azam UTV, leo Agosti 15, 2022 jijini Dar es Salaam. Kulia ni mtangazaji wa kipindi, Bw. Raymond Nyamwihula.

…………………..

Na Mwandishi Wetu, WHMTH,DAR ES SALAAM

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amewataka watanzania kutoa ushirikiano kwa makarani wa Sensa ya Watu na Makazi watakaopita kuchukua takwimu za watu na makazi siku ya taehe 23 Agosti 2022.

Waziri Nape ameyazungumza hayo leo Agosti 15, 2022 wakati wa alipotembelea kituo cha kurushia matangazo cha Azam Media Group na kushiriki kipindi cha Morning Trumpet cha Televisheni ya Azam UTV na kipindi cha Pevuka cha Redio ya UFM, jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa kuna taarifa nyingi zitakusanywa na makarani wa Sensa kwa lengo la kuisaidia Serikali kuweka mipango ya maendeleo inayozingatia idadi ya watu na makazi ili kufikisha huduma za kijamii kwa wananchi kulingana na uhitaji.

“Sensa ya Watu na Makazi ni jambo linalotokea mara moja kwa miaka kumi, ni muhimu kila mwananchi kushiriki katika zoezi hili, kwa kufanya hivyo utakuwa umejitendea haki wewe binafsi, jamii inayokuzunguka na Taifa kwa ujumla kwa kuisaidia Serikali katika mipango yake ya maendeleo”, Amezungumza Waziri Nape

 Ameongeza kuwa Serikali imedhamiria kuongeza ufanisi wa utendaji wake kupitia TEHAMA, na kudhihirisha hilo, Sensa itakayofanyika tarehe 23 Agosti 2022, itafanyika kidijitali kwa kutumia TEHAMA ambapo makarani wa Sensa watatumia vishikwambi kuingiza taarifa za watu na makazi ambazo zitaingia moja kwa moja kwenye mfumo.

“Tulikuwa tunatumia makaratasi kujaza takwimu za Sensa, safari hii hatutumii makaratasi na ndio faida ya TEHAMA, tutatumia vishikwambi kwa maana ya tablets na taarifa na takwimu zitakazochukuliwa zitaingizwa kwenye mfumo”, Amesisitiza Waziri Nape

“Takwimu zinaonesha zaidi ya asilimia 98 ya watanzania wanafahamu kuhusu Sensa inayoenda kufanyika, maandalizi ya Sensa yamekamilika kwa asilimia kubwa, mwananchi ambaye hatashiriki sensa hiyo atakuwa amejidhurumu haki yake lakini pia atakuwa hajaitendea haki nchi yake”, Amesisitiza Waziri huyo

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (kushoto), akizungumza katika kipindi cha Morning Trumpet cha Televisheni ya Azam UTV, leo Agosti 15, 2022 jijini Dar es Salaam. Kulia ni mtangazaji wa kipindi, Bw. Raymond Nyamwihula.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (kushoto), akizungumza katika kipindi cha Pevuka cha Redio ya UFM, leo Agosti 15, 2022 jijini Dar es Salaam. Kulia ni mtangazaji wa kipindi hicho, Bw. Ramadhan Tuwa.

  

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (kulia), alipotembelea studio za kurushia kipindi cha michezo cha Azam TV, leo Agosti 15, 2022 jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Meneja wa Mitambo wa Azam TV, Bw. Raghvendra Tiwari,

Matukio mbalimbali Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye (mwenye kaunda suti) alipotembelea ofisi za Azam Media Limited, leo Agosti 15, 2022 jijini Dar es Salaam.

About the author

mzalendoeditor