Featured Kitaifa

SERIKALI KUENDELEA NA UJENZI WA KIWANDA CHA DAWA NA VIFAATIBA, IDOFFI MAKAMBAKO – WAZIRI UMMY 

Written by mzalendoeditor

Na Englibert Kayombo – WAF, Njombe.

Serikali kuendelea na ujenzi wa Kiwanda cha uzalishaji Dawa na Vifaa tiba kilichopo chini ya Bohari ya Dawa (MSD), Idoffi -Makambako.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu leo alipokuwa akitoa salamu zake kwa wananchi wa Makambako mara baada ya kupewa nafasi hiyo kuzungumza kwenye Ziara Rais wa Jamhuri wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiwa Makambako- Njombe.

“Mheshimiwa Rais, hapa Makambako tunajenga kiwanda cha Dawa na Vifaa tiba ambapo ujenzi hapo nyuma ulisimama kwa tunarekebisha mambo kadhaa, lakini sasa tunaendelea na ujenzi” amesema Waziri Ummy Mwalimu.

“Nimesimama hapa kuwahakikishia wana makambako, Serikali itaendeleza na kukamilisha ujenzi wa kiwanda cha Dawa na Vifaa tiba ambacho kipo hapa Idoffi na tutaleta Shilingi Bilioni 17 kukamilisha ujenzi” Waziri Ummy amewahakikishia wananchi.

Waziri Ummy amesema Serikali imeshatoa kiasi cha Shilingi Bilioni 18 ikiwa ni kwa ajili ya ujenzi wa Kiwanda pamoja na kununua baadhi ya mashine za uzalishaji na hadi kukamilika kwa kiwanda hicho kutagharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 35.

Aidha, Waziri Ummy amesema Kiwanda hicho kitazalisha Dawa za vidonge (Tablets) Dawa za maji (Syrup) pamoja na mipira ya mikono (Gloves) huku kikitarajiwa kutoa ajira kwa watu zaidi ya 200.

About the author

mzalendoeditor