Featured Kitaifa

WAZIRI NDALICHAKO ATOA MAAGIZO MAZITO KWA WAMILIKI WA VIWANDA 

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akiangalia bidhaa ya sufuria inayotengenezwa na Kiwanda cha Nyakato Steel Mill Ltd wakati wa ziara yake iliyolenga kukagua utekelezaji wa sheria za kazi na Waajiri katika maeneo ya kazi. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na wafanyakazi wa Kiwanda cha kuchakata samaki cha Nile Perch kilichopo kata ya Nyakato, Wilaya ya Nyamagana Jijini Mwanza.

PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU

(KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU)

………………………………………..

Na: Mwandishi Wetu – MWANZA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amewataka wamiliki wa viwanda nchini kutekeleza ipasavyo sheria za kazi ikiwemo kuwapa mikataba ya kazi wafanyakazi wanaowaajiri ili kuepukana na migogoro mahali pa kazi.

Akiongea baada ya kufanya ziara ya kukagua utekelezaji wa sheria za kazi na Waajiri katika maeneo ya kazi ya viwandani jijini Mwanza, Waziri Ndalichako amefafanua kuwa suala kubwa alilobaini katika ziara hiyo kuwa wapo wafanyakazi ambao hawana mikataba kabisa ya kazi aidha ya kudumu au ya muda mfupi.

“Wafanyakazi wengine wameajiriwa kwa zaidi ya miaka kumi na tano lakini wanakuwa wanapewa mkataba wa mwezi mmoja mmoja, sheria za mikataba ya wafanyakazi zinaweka wazi juu ya aina ya kazi ambazo mfanyakazi anaweza kupewa mkataba wa kudumu au wa muda mfupi, Mikataba mingine huandaliwa tu kwa ajili ya kutuonesha watendaji wa serikali lakini wafanyakazi hawana nakala hizo na hata wakati wa kusaini wafanyakazi hawajui kilichomo ndani ya hiyo mikataba,” alisema Waziri Ndalichako

Aidha, amesisitiza kuwa suala la Usalama na Afya mahala pa kazi bado ni changamoto katika viwanda vingi hususan katika kuwapatia vifaa kinga wafanyakazi wakati wa shughuli za uzalishaji viwandani, hivyo amefafanua kuwa Ofisi hiyo kupitia OSHA itaendelea kutoa elimu ili kuhakikisha sheria ya Usalama na Afya mahala pa kazi inatekelezwa.

Mhe. Ndalichako amefafanua kuwa utekelezaji wa sheria za kazi katika viwanda hivyo umeongezeka kwa kulinganisha na kaguzi zilizopita japokuwa bado kuna mapungufu hususan katika kulipa michango ya wafanyakazi kwenye mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

“Ni wasihi waajiri wahakikishe wanakuwa na takwimu sahihi za michango wanayowasilisha katika mifuko ya hifadhi ya jamii, kwani idadi ya wafanyakazi wanaochangiwa katika mfuko wa NSSF tumekuta inakuwa tofauti sambamba na michango ya mfuko wa WCF, ikiwa idadi ya wafanyakazi walio ajiriwa ipo hivyo, mnapaswa kuhakikisha takwimu hiyo inaoana na waliochangiwa katika mifuko ya Hifadhi ya jamii” alieleza

Aliongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeendelea kuvutia wawekezaji nchini kwa lengo la kuongeza fursa za ajira kwa wananchi.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Mwanza, amemuhakikishia Mhe. Waziri kuwa watahakikisha wanashirikiana na watendaji wanao husika na masuala ya kusimamia sheria za kazi mkoani humo kwa lengo la kutekeleza maagizo yake kwa wakati.

Katika hatua nyingine, Menejimenti za Viwanda vilivyotembelewa zimeshukuru kwa ushirikiano wanaoupata kutoka katika Taasisi za serikali hususan katika utekelezaji wa sheria za kazi, suala ambalo huwasaidia katika uzalishaji wao kuwa wa tija. Aidha, wameahidi kutelekeleza maagizo waliyopewa kikamilifu ili kuepukana na migogoro katika viwanda vyao.

About the author

mzalendoeditor