Featured Kitaifa

WAZIRI MAKAMBA:”SERIKALI HAISAMBAZI UMEME KWA AJILI YA KUWASHA TAA PEKEE”

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba (wa pili kutoka) akizungumza na Meneja wa Kiwanda cha KUZA Afrika, Rob Clowes ambacho kinachakata maparachichi ili kutengeneza mafuta na bidhaa nyingine wilayani Rungwe mkoani Mbeya. Kiwanda hicho kinafanya uzalishaji kwa kutumia umeme uliunganishwa na TANESCO.

Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba akifungua valvu ili kuruhusu majimoto yanayotoka ardhini kupita katika kisima kifupi cha utafiti wa Jotoardhi kilichochorongwa katika eneo la Kiejo-Mbaka wilayani Rungwe mkoani Mbeya.

………………………

Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba amesema kuwa, Serikali haisambazi umeme vijijini kwa ajili ya kuwasha taa peke yake bali kuchagiza pia shughuli za kiuchumi ikiwemo uanzishaji  wa viwanda.

Amesema hayo tarehe 28 Julai, 2022 baada ya kutembelea kiwanda kinachochakata  parachichi  ili kutengeneza mafuta  cha KUZA AFRIKA kilichopo wilayani Rungwe Mkoa wa Mbeya mbacho  kimeunganishiwa umeme na  Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO). 

Makamba alisema kuwa, uwepo wa kiwanda hicho  ni matokeo ya uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika sekta ya Nishati ambao umezaa matunda kwani kiwanda hicho pamoja na kuongezea thamani  mazao ya Wakulima, kimezalisha ajira zaidi ya 200 ndani ya kiwanda na katika mashamba ya parachichi.

Aliongeza kuwa, msingi mzima wa kupeleka umeme vijijini ni kusawazisha maendeleo kati ya watu wa vijijini na mijini kwani shughuli za kiuchumi kama za viwanda zinaboresha pia uchumi wa wananchi wa vijijini. 

Meneja wa TANESCO, Wilaya ya Rungwe, Mhandisi Mukhsin Kijemkuu alimweleza Waziri wa Nishati kuwa, kiwanda  hicho kabla ya kufungiwa transforma yake kilikuwa kikizalisha lita 2000 kwa siku lakini baada ya kupata Transfoma wiki moja iliyopita kinazalisha lita 4000 kwa siku. 

Aliongeza  kuwa kwa lita 4000 zinazotarajiwa kuzalishwa kwenye kiwanda hicho mwekezaji angetumia shilingi milioni 50 kununua dizeli ya kuendesha mitambo ila kwa kuwa sasa anatumia takriban shilingi milioni 30 kwa gharama za umeme ambayo ni pungufu ya gharama alizokuwa akiingia awali.

Pamoja na kuishukuru Wizara ya Nishati kwa kutenga fedha za kupeleka umeme kwenye maeneo kama hayo, Mhandisi Kijemkuu amekaribisha wawekezaji wengine kuwekeza kwenye miradi kama hiyo kwani hali ya upatikanaji umeme sasa imeimarika na pia TANESCO itaongeza mapato yake.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Nishati alifika kwenye Kijiji cha Iramba Kata ya Ntaba wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya ili kukagua kazi zinazoendelea katika chanzo cha Jotoardhi  cha Kiejo-Mbaka ambacho kinatarajiwa kuzalisha umeme utakaoingizwa kwenye gridi ya Taifa.

Waziri Makamba mara baada ya kukagua chanzo hicho, alisema kuwa “Serikali imeamua kuweka nguvu katika kuzalisha umeme kwa njia mbalimbali, tuna umeme wa Maji, Umeme wa Gesi na safari hii tumewekeza kwenye umeme wa Joto ardhi, hapa Kiejo-Mbaka ni moja ya vyanzo vya Jotoardhi ambavyo vina uwezekano wa kuzalisha umeme wa Joto ardhi.”

Alisema kuwa katika bajeti ya Wizara ya Nishati ya mwaka 2022/2023, Serikali imetenga shilingi Bilioni 5  kwa ajili ya kuendeleza miradi hiyo  na kwamba Serikali imenunua mtambo maalum wa kuchoronga mpaka Kilometa 3 chini ili kuweza kulifikia joto ambalo litatoa mvuke utakaozungusha mtambo wa kuzalisha umeme.

Aliongeza kuwa, matarajio ni kuzalisha umeme wa kiasi cha megawati 200 ifikapo mwaka 2025 huku akitaja kuwa Tanzania kuna maeneo mengi yanayoweza kutoa nishati ya Jotoardhi ya kiasi cha megawati 5000.

Licha ya kuzalisha umeme, alitaja faida nyingine za Jotoardhi kuwa ni pamoja na ukaushaji wa mazao na kupasha moto nyumba kitalu ili kuongeza thamani ya mazao na ufugaji wa samaki kwani maji yanayotokana na jotoardhi hutumika kuongeza joto katika bwawa la samaki katika mazingira ya baridi na hivyo kupelekea samaki kukua kwa haraka.

Nishati ya Jotoardhi inatokana na joto linalotoka kwenye mwamba wenye joto  unaochemsha maji yaliyoingia ardhini.

About the author

mzalendoeditor