Featured Kitaifa

MWENGE WA UHURU KUPOKELEWA JULAI 26 MWAKITOLYO SHINYANGA

Written by mzalendoeditor

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akizungumza na waandishi wa habari juu ya ujio wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Halmashauri ya Shinyanga na Manispaa ya Shinyanga Julai 26 hadi 27 ambapo Julai 28 wataukabidhi wilayani Kishapu. 

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

MKUU wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, ametoa wito kwa wananchi wajitokeze kwa wingi kuupokea Mwenge wa Uhuru  mkoani Shinyanga ambao utapokelewa Julai 26 katika Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kata ya Mwakitolyo ukitokea mkoani Geita.

Ametoa wito huo leo Julai 23, 2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake.

“Mwenge huu wa Uhuru katika Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga utakesha kwenye viwanja vya Stendi ya Mabasi Iselamagazi, Manispaa ya Shinyanga ni viwanja vya Sabasaba, naomba Wafanyabiashara, Wajasiriamali wachangamkie fursa hii kufanya biashara,”amesema Mboneko.
 

“Kwenye Mikesha hii kutakuwa na ulinzi wa kutosha na tumejipanga vizuri kuhakikisha usalama wa wananchi una kuwepo, na hakuna fujo yoyote ambayo itatokea wala viashiria vya uvunjifu wa amani, na ninaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kwenye Mbio hizi za Mwenge wa uhuru,”ameongeza Mboneko.

Amesema Mwenge huo utapita katika Barabara za Bushushu, Ibadakuli, Katemi, Empire, Hospitali ya Mkoa, Mazingira Center , Soko kuu, Shycom, Japanize kona hadi viwanja vya Sabasaba kwenye eneo la Mkesha, na kuwaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kwenye Barabara hizo kuupokea Mwenge na kuushangilia, ambapo Julai 28 wataukabidhi wilayani Kishapu.
 

 Amesema katika wilaya ya Shinyanga, Mwenge huo wa Uhuru utakimbizwa Kilomita 100 na kuzindua Mradi mmoja pamoja na kuweka jiwe la Msingi kwenye Miradi Minne jumla inakuwa miradi mitano.

Ametaja Miradi hiyo, kuwa ni Mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria uliopo Mwakitolyo ambao utanufaisha wananchi 14,000, Mradi mwingine ni kituo cha Mafuta cha mtu binafsi, kuweka pia jiwe la Msingi Jengo la wagonjwa wa dharura katika Hospitali ya wilaya, na nyumba nne za watumishi, pamoja na kuzindua Klabu ya Mazingira ya wanafunzi shule ya Msingi Iselamagazi.

Amesema katika Manispaa ya Shinyanga Mwenge huo wa Uhuru pia utakimbizwa Kilomita 102 na kuzindua Miradi miwili, na mingine miwili kuwekewa jiwe la msingi huku mradi mmoja ukikaguliwa na kushiriki shughuli za ujenzi jumla inakuwa mitano.

Mboneko ameitaja Miradi hiyo kwa Manispaa ya Shinyanga, kuwa ujenzi wa Zahanati ya Bushushu na mradi wa Maji Ziwa Victoria katika kijiji cha Bugwandege Kata ya Ibadakuli ambapo miradi hiyo yote itazinduliwa.

Amesema katika Miradi mingine miwili ya ujenzi wa vyumba vya Madarasa Sita na Ofisi Mbili za walimu Shule ya Msingi Bugweto, pamoja na kiwanda cha bia cha mtu binafsi yenyewe itawekewa jiwe la msingi.

Pia ameutaja mradi wa tano kuwa ni kukagua na kushiriki ujenzi wa Jengo la Utawala la Manispaa ya Shinyanga, na kubainisha kuwa Mbio hizo za Mwenge wa Uhuru katika Halmashauri zote hizo mbili utakimbizwa Kilomita 202 na thamani ya miradi yote ni Sh.bilioni 33.1.

Kauli Mbiu ya Mwenge wa Uhuru mwaka huu( 2022), inasema Sensa ni Msingi wa Mipango ya Maendeleo: Shiriki kuhesabiwa, tuyafikie Maendeleo ya Taifa.

About the author

mzalendoeditor