Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameiagiza Wizara ya Afya kubaini maeneo yenye upungufu mkubwa wa wataalamu wa famasi na kupendekeza namna ya kuwaajiri kwa awamu kulingana na bajeti. Ametoa agizo hilo leo, tarehe 25 Novemba 2026, akifungua Kongamano la Kisayansi na Mkutano Mkuu wa 56 wa Chama cha Wafamasia Tanzania katika ukumbi wa Kwatunza Beach, jijini Mwanza.
Ndejembi ameitaka Wizara ya Afya kushirikiana na Ofisi ya Rais – UTUMISHI kukamilisha maboresho ya ikama ili kutambua ubobezi katika kada za afya, ikiwemo famasi. Amesisitiza umuhimu wa kuendana na wakati wa sasa kwa kuanzisha kurugenzi ya dawa katika Wizara ya Afya, pamoja na muundo wa kurugenzi unaofaa katika hospitali ya Taifa, hospitali za kanda na hospitali maalum.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Makamu wa Rais, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amesema Serikali imetenga ekari 400 Mloganzila kwa ajili ya kongani ya viwanda vya dawa. Amesema viwanda sita vinaendelea kujengwa na baadhi vinatarajiwa kuanza uzalishaji mwaka 2027.
Rais wa Chama cha Wafamasia Tanzania, Mfamasia Fadhil Hezekiah, Ameomba mapitio ya ikama yazingatie majukumu ya sasa ya wafamasia, yakiwemo kutoa huduma katika kliniki za magonjwa sugu, kusimamia ugavi na kufuatilia usalama wa dawa.







