Jumanne, Novemba 24, 2026
HABARI MPYA
Michezo

MUDRYK: ARSENAL NDIO ILIKUWA NDOTO YANGU, SI CHELSEA

Na.Mwandishi Wetu,MZALENDO BLOG

WINGA wa Chelsea, Mykhaylo Mudryk, amefichua kuwa ndoto yake kubwa kabla ya kujiunga na klabu hiyo ilikuwa kucheza Arsenal, akidai wakala wake wa zamani alihusika kuvuruga mpango huo kwa kutanguliza maslahi ya kifedha badala ya matakwa yake.

Mudryk amesema Arsenal ilikuwa klabu aliyokuwa na shauku kubwa ya kuichezea, huku akitamani kuvaa jezi ya timu hiyo na kucheza katika Uwanja wa Emirates, lakini hakukuwa na juhudi za kutosha kutoka kwa wakala wake wa zamani kuhakikisha ndoto hiyo inatimia.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na kipindi cha Guest of Gordon, winga huyo raia wa Ukraine amesema nia yake ya kujiunga na Arsenal haikuwa siri kwa watu waliokuwa karibu naye, akieleza kuwa alitamani kuhamia Emirates kabla ya  kutua Stamford Bridge.

“Kabla ya kwenda Chelsea, nilitaka kujiunga na Arsenal. Hiyo si siri. Arsenal ilikuwa klabu niliyotaka kuichezea na kuhamia Emirates ilikuwa ndoto yangu,” amesema Mudryk.

Ameongeza kuwa hakukuwa na jitihada za dhati za kutimiza matakwa yake, akidai wakala wake wa zamani alikuwa akijikita zaidi katika kuhakikisha anapata fedha nyingi kupitia dili hilo la uhamisho.

Mudryk amesema wakati mazungumzo ya uhamisho yakiendelea hakuwa akifahamu mambo yaliyokuwa yakifanyika nyuma ya pazia, ikiwemo masuala ya kamisheni na maslahi ya kifedha yaliyohusishwa na dili hilo.

“Niliyafahamu masuala ya kamisheni na mambo mengine yote baadaye. Wakati huo sikujua kilichokuwa kinaendelea,” amesema.

Kauli hiyo imeibua upya simulizi za uhamisho wake kutoka Shakhtar Donetsk ya Ukraine kwenda Chelsea Januari 2023, wakati Arsenal nayo ilikuwa ikihusishwa kwa karibu na harakati za kumsajili nyota huyo.

Mudryk alijiunga na Chelsea kwa mkataba wa muda mrefu, licha ya awali kuhusishwa na uwezekano wa kutua Arsenal, jambo ambalo sasa ameeleza kuwa lilikuwa kinyume na ndoto yake ya wakati huo.