Featured • Kitaifa

TANZANIA YAJIPANGA KUHAMIA MFUMO WA KIMATAIFA WA UAINISHAJI WA MAGONJWA ICD-11

Written by Alex Sonna

Na Atley Kuni, WAF-DODOMA

Wizara ya Afya imetabaisha umuhimu wa kuhamia katika mfumo mpya wa kimataifa wa uainishaji wa magonjwa (ICD-11), kutoka mfumo wa sasa wa ICD-10, ili kuboresha usahihi wa takwimu za magonjwa na vifo, kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa na kuongeza ufanisi wa mipango na utoaji wa huduma za afya nchini.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali Dkt.Eliudi Eliakimu, wakati wa ufunguzi wa kikao cha wadau cha kujadili matokeo ya tathmini ya utayari wa Tanzania kuhamia mfumo huo, iliyofanyika Novemba 20, 2026, jijini Dodoma, Dkt.Eliakimu amesema mabadiliko hayo ni fursa muhimu ya kuimarisha ubora na ulinganifu wa takwimu za afya kitaifa na kimataifa.

“Tathmini iliyofanyika Septemba 2026 imeonesha kuwa Tanzania ina msingi mzuri wa mifumo ya afya ya kidijitali na uwezo wa mifumo hiyo kuwasiliana, lakini bado kuna maeneo yanayohitaji kuimarishwa kabla ya utekelezaji wa ICD-11”, amesema Dkt. Eliamimu.

Dkt. Eliakimu ameanisha baadhi ya changamoto kuwa ni pamoja na uandishi na uthibitishaji wa taarifa za chanzo cha vifo, ujuzi wa wataalamu katika uainishaji wa magonjwa, matumizi ya mifumo sanifu ya utoaji taarifa na kuoanisha mifumo ya taarifa za afya na ulipaji wa huduma.

Aidha, amesisitiza kuwa kuhamia mfumo huo kunahitaji maandalizi ya pamoja, ikiwemo kuimarisha mifumo ya usimamizi, kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya, kufanya maboresho ya mifumo ya TEHAMA na kuweka mikakati ya kulinda ubora wa takwimu za afya.

Ametumia fursa hiyi kuwataka wadau wote kushirikiana kwenye kuandaa mpango kazi wa kitaifa wa utekelezaji wa ICD-11, pamoja na kuunga mkono upatikanaji wa rasilimali fedha kupitia bajeti ya ndani na ushirikiano na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha mabadiliko hayo yanafanyika kwa ufanisi na endelevu.

Kikao hicho kimewashirikisha Wizara ya Afya, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), Benki ya Dunia, UNICEF, taasisi za utafiti na wadau wengine wa sekta ya afya, kimekusudia kujadili matokeo ya tathmini na kuweka vipaumbele vitakavyoongoza utekelezaji wa mfumo wa ICD-11 nchini.

About the author

Alex Sonna