Na Jackline Minja, WMJJWM
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, amewaomba Wabunge wanaporejea majimboni kuhamasisha na kusaidia uanzishwaji wa sheria ndogo ndogo zitakazoimarisha malezi ya watoto na vijana katika jamii ili kulinda na kudumisha maadili ya nchi.
Amesema hayo wakati akijbu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Najma Murtaza Giga, aliyetaka kujua kwa nini Serikali haitungi Sera ya Taifa ya Malezi kwa Watoto na Vijana ili kukabiliana na kuporomoka kwa maadili, Mahundi ameeleza kuwa Serikali haijaona umuhimu wa kuwa na sera inayojitegemea kwa kuwa masuala ya malezi na maadili tayari yamejumuishwa katika sera na sheria mbalimbali za kisekta.
“Ni umuhimu wa kuweka mifumo imara ya malezi kuanzia ngazi ya familia hadi jamii, ili kuhakikisha watoto na vijana wanalelewa katika misingi inayozingatia maadili, uwajibikaji na utamaduni wa Kitanzani” amesema Maryprica
Amezitaja sera na sheria hizo kuwa ni Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008, Sheria ya Mtoto Sura ya 13 pamoja na Sera ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007, ambazo zinaweka misingi ya kushughulikia masuala ya malezi, makuzi na maendeleo ya watoto na vijana nchini.
Aidha, ameeleza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza miongozo na programu mbalimbali za kitaifa ikiwemo Programu Jumuishi ya Malezi na Makuzi (PJT-MMMAM), Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) pamoja na Programu ya Ulinzi na Usalama wa Mtoto Mitandaoni.
Vilevile, amebainisha kuwa Serikali inaendelea kufanya mapitio ya Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008 ili kuingiza masuala ya kisasa, yakiwemo udhibiti wa athari za teknolojia, hatua inayolenga kuimarisha zaidi misingi ya malezi, ulinzi na maadili kwa watoto nchini.