Featured • Kitaifa

MIRADI YA UMEME VIJIJINI IMEBORESHA HUDUMA ZA KIJAMII – UJUMBE BENKI YA DUNIA

Written by Alex Sonna

 

Na.Mwandishi Wetu-Mwanza

Benki ya Dunia yapongeza miradi ya umeme vijijini kwa kuboresha maisha ya wananchi vijijini pamoja na huduma za kijamii.

Pongezi hizo zimetolewa leo na Mtaalam Mwandamizi wa Fedha kutoka Benki ya Dunia, Nkundwe Mwakiluma wakati wa ziara ya Ujumbe kutoka Benki ya Dunia iliyolenga kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na Benki hiyo na kusimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

“Tumefurahi sana kama Benki ya Dunia kufika hapa, lakini kikubwa zaidi tumefurahi kuona mafanikio ambayo uunganishaji wa umeme umeleta katika kituo hiki cha Afya. Tumefurahi kuona fedha tuliyochangia kama sehemu ya mradi wa kupeleka umeme vijijini kimeleta mabadiliko makubwa na mafanikio makubwa kwenye sekta ya Afya,” amesema Mwakiluma mara baada ya kutembelea Kituo cha Afya cha Lushamba kilichopo katika Wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza.

Awali akitoa taarifa kuhusu utekelezwaji wa mradi huo, Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu na Teknolojia Mbadala kutoka REA, Mhandisi Advera Mwijage amesema Benki ya Dunia imekuwa ni mdau muhimu katika utekelezaji wa miradi ya Nishati Vijijini ukiwepo mradi wa kufikisha umeme vijijini.

Mhandisi Mwijage amesema kuwa Kituo hicho cha Afya awali kilikuwa ni Zahanati kabla ya kupandishwa hadhi na kuwa Kituo cha Afya baada ya kupata umeme kupitia miradi inayotekelezwa na REA.

“Tumeshuhudia mashine mbalimbali ambazo hazikuwepo awali kabla ya kufikishiwa umeme. Uwepo wa umeme umeweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma za afya sehemu mbalimbali nchini kama ilivyo hapa. Hizi ni juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali kwa kushirikiana na Wabia mbalimbali wa Maendeleo kama Benki ya Dunia katika kuboresha maisha ya wananchi,” amesema Mhandisi Mwijage.

Mhandisi Mwijage amewashukuru Wabia wa Maendeleo wakiwamo Benki ya Dunia kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezwaji wa miradi mbalimbali ya nishati vijijini huku akiahidi kuwa wataendelea kusimamia fedha zinazotolewa kwa usahihi ili kuweza kuleta matokeo chanya kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Bw. Simon Masasi pamoja na Bi. Adventina Pascal ni wakazi wa Kijiji cha Irigamba wamesema kuwa uwepo wa umeme katika Kituo hicho cha Afya kumewaondolea adha ya kusafiri umbali wa saa Nne kwenda kupata huduma za baadhi ya vipimo mjini ambavyo walikuwa hawawezi kuvipata katika Kituo hicho hapo awali kabla ya kupata umeme.

    

About the author

Alex Sonna