Na Mwandishi wetu, DODOMA
CHANGAMOTO ya upatikanaji wa mitaji inayowakabili wanawake wanaojishughulisha na biashara ndogo ndogo jijini Dodoma imepata nafuu kwa baadhi yao baada ya wajasiriamali 1,450 kufikiwa na mikopo inayotolewa kupitia ushirikiano wa Self Microfinance Fund (SELF MF),na Wodesu Microcredit, unaolenga kuwapa nafasi ya kuimarisha biashara, kuongeza kipato na kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa Bodi ya SELF MF jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa Wodesu Microcredit, Melina Faustine, amesema ushirikiano huo umeongeza uwezo wa taasisi yake kuwafikia wanawake wengi zaidi, wakiwemo wanaouza mboga za majani ambao wamekuwa wakikabiliwa na ugumu wa kupata mikopo katika baadhi ya taasisi za kifedha.
Amesema miongoni mwa walionufaika na fursa hiyo ni wanawake wanaouza mboga za majani, ambao wamekuwa wakihitaji mitaji ili kuendeleza shughuli zao za kujipatia kipato.
“Kupitia mikopo ya SELF MF nimeweza kuwafikia wanawake 1,450, wakiwemo wale wanaouza mboga za majani ambao si rahisi kupata mikopo katika sehemu nyingine,” amesema Faustine.
Hata hivyo, amebainisha kuwa baadhi ya waombaji wa mikopo wamekuwa wakiwasilisha taarifa za biashara ambazo si zao, akionya kuwa tabia hiyo inaweza kuathiri matumizi sahihi ya fedha na kusababisha changamoto katika urejeshaji wa mikopo.
Amesisitiza umuhimu wa waombaji kutoa taarifa sahihi na za kweli ili kuhakikisha mikopo inawafikia walengwa na kutumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa, hatua itakayosaidia kuimarisha marejesho na kuwezesha wajasiriamali wengine kunufaika na huduma hizo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya SELF MF, Paul Sangawa, amesema ziara hiyo imelenga kujionea utekelezaji wa ushirikiano kati ya mfuko huo na taasisi za kifedha katika kusogeza huduma za mikopo karibu na wananchi.
Amesema taasisi kama Wodesu Microcredit zina mchango muhimu katika kuwafikia wafanyabiashara wadogo, hususan wanawake wanaohitaji mitaji ya kuanzisha, kuimarisha na kupanua biashara zao.
Sangawa amesisitiza kuwa usimamizi mzuri wa mikopo, ufuatiliaji wa matumizi yake na urejeshaji kwa wakati ni muhimu katika kuhakikisha fedha hizo zinaendelea kuwanufaisha wananchi wengine wenye mahitaji ya mitaji.
“Wananchi wengi wana mahitaji ya mikopo na hii ni mojawapo ya fursa wanazoweza kuzitumia kujikwamua kiuchumi na kuanzisha shughuli mbalimbali zinazoweza kuwasaidia kuboresha maisha yao,” amesema.
Naye Msemaji Mkuu wa SELF MF, Santieli Yona, amesema mfuko huo una aina mbalimbali za mikopo zinazolenga kukidhi mahitaji ya makundi tofauti ya wananchi, wakiwemo wakulima, wafanyabiashara na wafanyakazi wa Serikali, pamoja na kusaidia taasisi za kifedha kupanua huduma zake.
Amesema SELF MF hutoa mikopo kwa taasisi za kifedha zilizosajiliwa kisheria, vyama vya kuweka na kukopa (SACCOS), pamoja na mikopo ya moja kwa moja kwa watu binafsi, kulingana na aina ya huduma na vigezo vilivyowekwa.
Yona amewahimiza Watanzania kutumia fursa hizo kwa kuzingatia masharti ya mikopo na kuandaa mipango madhubuti ya biashara itakayowawezesha kutumia mitaji kwa tija na kurejesha fedha kwa wakati.
“Tunakaribisha Watanzania wote waje SELF MF kwa sababu tuna mikopo ya aina mbalimbali kwa ajili ya biashara na shughuli tofauti za kiuchumi. Lengo letu ni kuwawezesha wananchi kupata mitaji ya kuendeleza shughuli zao,” amesema.
Ameongeza kuwa uelewa wa masharti ya mikopo na usimamizi bora wa fedha ni nguzo muhimu katika kuhakikisha mikopo inachochea ukuaji wa biashara, kuongeza kipato na kuimarisha ustawi wa wananchi.
