Featured • Kitaifa

KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA WATUMISHI HOUSING

Written by Alex Sonna

Na Alex Sonna, DODOMA

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imeridhishwa na utekelezaji wa miradi ya nyumba zinazojengwa na Watumishi Housing Investments (WHI) kwa ajili ya watumishi wa umma, ikipongeza kasi ya ujenzi, ubora wa majengo na hatua ya kutoa karibu nyumba 1,500 kwa watumishi wa umma.

Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Edwin Enosy Swalle, amesema hayo wakati wa ziara ya kamati hiyo ya kutembelea na kukagua miradi ya nyumba zinazotekelezwa katika eneo la Mradi wa watumishi Housing Investment uliopo Njedengwa na Mradi wa Mlezi kwa ajili ya watumishi wa umma.

Amesema utekelezaji wa miradi hiyo unaonesha juhudi za Serikali katika kuboresha makazi ya watumishi wa umma na kutekeleza dhamira ya kuboresha ustawi wao, akieleza kuwa watumishi wanapopata makazi bora, mazingira yao ya kazi na utoaji wa huduma kwa wananchi huimarika.

“Kamati ya Bunge imeridhika sana na utayari na kasi ya watumishi Housing Investment ya kuinua hali ya makazi ya watumishi wa umma nchini. Tumeona spidi ya majengo mnayojenga, ubora wake na taarifa kwamba mmetoa nyumba karibu 1,500 kwa ajili ya watumishi wa umma,” amesema Mhe.Swalle.

Amesema pamoja na mafanikio hayo, ongezeko la idadi ya watu nchini huku ardhi ikiwa rasilimali isiyoongezeka linapaswa kuifanya Watumishi Housing Investment kuweka kipaumbele katika kutafuta na kuhifadhi maeneo kwa ajili ya miradi ya sasa na ya baadaye.

Amesisitiza umuhimu wa kuwa na benki ya ardhi itakayowezesha taasisi hiyo kuwa na uhakika wa maeneo ya kujenga nyumba, ili kuendeleza huduma kwa watumishi wa umma na kuhakikisha miradi hiyo inakuwa endelevu kwa vizazi vijavyo.

Katika hatua nyingine, Mhe.Swalle ameipongeza taasisi hiyo kwa kuhamasisha watumishi kujiunga na mfuko wa uwekezaji wa Faida Fund, akisema taarifa iliyowasilishwa kwa kamati inaonesha kuwa watumishi zaidi ya 4,000 walikuwa wameanza kuchangia na kufikia Juni 2026, michango yao ilikuwa imezidi Sh bilioni 1.2.

Hata hivyo, amesema bado kuna haja ya kuongeza elimu kuhusu mfuko huo kwa watumishi wengi zaidi ili waelewe manufaa yake ya kiuchumi wa mtu mmoja mmoja na kukuza vipato vyao.

Kuhusu upatikanaji wa makazi, amesema kamati imebaini kuwa Watumishi Housing Investment inatekeleza miradi ya nyumba zinazouzwa kwa watumishi pamoja na nyumba zinazotolewa bure kwa ajili ya kuishi kwa watumishi wanaostahili wilayani.

Amesema ujenzi wa nyumba za watumishi wa umma wilayani unapaswa kupewa kipaumbele zaidi, hasa katika halmashauri na maeneo ambayo watumishi wanakabiliwa na changamoto ya kupata makazi ya uhakika.

Kwa mujibu wa Swalle, changamoto ya makazi inaweza kuchangia watumishi kuomba uhamisho kutoka maeneo yenye mazingira magumu, hivyo kuathiri upatikanaji wa watumishi katika maeneo hayo.

Aidha, ameitaka taasisi hiyo kuweka utaratibu madhubuti wa kusimamia nyumba zinazotolewa bure ili kuhakikisha zinawanufaisha watumishi wanaostahili na kuzuia uwezekano wa nyumba hizo kutumiwa kwa shughuli za kibiashara, ikiwemo kupangishwa kwa watu wengine kinyume na malengo yaliyokusudiwa.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete, amesema WHI wamekamilisha ujenzi wa nyumba 54 kwa ajili ya watumishi wa umma waliopo katika mazingira magumu, huku ujenzi wa nyumba nyingine 78 ukifikia asilimia 87 na nyumba 66 katika eneo la Kisasa Hilltop, Njedengwa jijini Dodoma ukiwa umefikia asilimia 45.

Amesema nyumba 54 zilizokamilika zimejengwa katika mikoa ya Singida, Dodoma, Pwani, Ruvuma na Lindi, kwa lengo la kuwawezesha watumishi wa umma wanaofanya kazi katika mazingira magumu kupata makazi salama na kuboresha mazingira yao ya utendaji kazi.

“WHI inaendelea na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa nyumba 78 katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Mbeya, Dodoma na Kigoma.”ameeleza Waziri Kikwete

Amesema hadi Juni 2026, utekelezaji wa mradi huo ulikuwa umefikia asilimia 76, huku maendeleo ya ujenzi yakifikia asilimia 87 wakati wa taarifa hiyo.

Katika hatua nyingine, Mhe. Kikwete amebainisha kuwa WHI inaendelea na ujenzi wa nyumba 66 katika eneo la Kisasa Hilltop, Njedengwa jijini Dodoma, mradi ulioanza katika mwaka wa fedha 2025/2026.

Kwa mujibu wa maelezo hayo, hadi Juni 2026 mradi huo ulikuwa umefikia asilimia 45 ya utekelezaji, huku ujenzi wa nguzo na sakafu ukiwa umekamilika na kazi nyingine zikiendelea. Mradi huo unatarajiwa kukamilika Februari 2027.


Awali Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Watumishi Housing Investments (WHI) Arch.Sephania Solomon,amesema kuwa taasisi hiyo inaendelea kupitia na kuboresha miundombinu ya majengo yake ili kukidhi mahitaji ya makundi mbalimbali ya watumishi , kwa kuzingatia ushauri uliotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ili yaweze kutumika kirahisi na watu wenye mahitaji maalumu.

Aidha, amesema kuwa katika “Mradi wa nyumba za gharama nafuu za Njedengwa, awamu ya kwanza ya ujenzi inatarajiwa kukamilika Februari 2027, wakati awamu nyingine zikiendelea kutekelezwa kwa mujibu wa mpango. Ameongeza kuwa mwitikio wa wanunuzi umeoneshwa kupitia ahadi za malipo ya awali ya asilimia 30, hatua inayolenga kusaidia kuendeleza ujenzi wa nyumba hizo.”amesema Arch.Solomon

Ameeleza kuwa WHI itaendelea kutoa taarifa za kina kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo, ikiwemo maendeleo ya ujenzi, mpango wa uendelezaji wa nyumba na idadi ya nyumba zilizobaki kupatikana. Hatua hizo zinalenga kuimarisha uwazi, kuongeza uelewa wa wadau na kuwezesha wananchi kupata taarifa sahihi kuhusu fursa za kumiliki nyumba za gharama nafuu.

 

 

About the author

Alex Sonna