Morogoro,
Wizara ya Nishati imewajengea uwezo viongozi wa Umoja wa Mamalishe na Babalishe Tanzania (UMALITA) kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo katika shughuli za biashara na maisha ya kila siku.
Mafunzo hayo yametolewa leo, Oktoba 15, 2026, mkoani Morogoro, yakilenga kuongeza uelewa wa viongozi hao kuhusu teknolojia mbalimbali za nishati safi ya kupikia, matumizi salama pamoja na fursa za kifedha za kupata vifaa vinavyotumia nishati hiyo.
Akifungua mafunzo hayo, Mjiolojia Mkuu kutoka Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia Wizara ya Nishati, Ngereja Mgejwa, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na wadau katika kuhamasisha mamalishe na babalishe kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na kuhamia kwenye nishati safi ya kupikia.
Amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024–2034, unaolenga kufikia asilimia 80 ya Watanzania wanaotumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Aidha, Mgejwa ameeleza kuwa matumizi ya kuni na mkaa yanaweza kusababisha athari kwa afya, mazingira na uchumi wa wananchi, hivyo kusisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kuhusu faida za nishati safi ya kupikia, hususan kwa mamalishe na babalishe wanaotumia nishati kwa kiwango kikubwa katika shughuli zao za biashara.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Aprili 21, 2026, wakati wa Kongamano la UMALITA, ambapo Wizara ya Nishati ilielekezwa kuweka mikakati mahsusi ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa mamalishe na babalishe nchini.
Kupitia mafunzo hayo, viongozi wa UMALITA wanatarajiwa kutumia maarifa watakayoyapata kuelimisha na kuhamasisha wanachama wao katika maeneo mbalimbali nchini, hatua inayotarajiwa kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuchangia kufikiwa kwa lengo la Taifa la asilimia 80 ifikapo mwaka 2034.
