Featured • Kitaifa

‎MAKAMU WA RAIS AAGIZA MIFUMO YA FURSA ZA VIJANA KUSOMANA

Written by Alex Sonna

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, akizungumza na Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano alipotembelea banda la ofisi hiyo leo Oktoba 14, 2026 katika Maonesho ya Wiki ya Vijana yaliyofanyika, Sumbawanga, mkoani Rukwa.
‎
‎Na: Mwandishi Wetu, Rukwa
‎
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ametaka mifumo ya kidijitali ya Serikali inayotoa taarifa za ajira na fursa kwa vijana kuunganishwa ili iweze kusomana na kubadilishana taarifa kwa urahisi.

Amesema hayo leo alipotembelea banda la Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano katika Maonesho ya Wiki ya Vijana yanayoendelea Shule ya Msingi Ndua, Sumbawanga, mkoani Rukwa.

Amesema Serikali ni moja, hivyo mifumo iliyopo Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano na Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana inapaswa kuunganishwa ili fursa zote zikusanywe pamoja na kupelekwa kwa vijana.
‎
‎Halikadhalika Mhe. Ndejembi, amesema kuwa muda alioutoa kwa ajili ya kutekeleza maelekezo aliyoyatoa jijini Arusha Septemba 28, 2026, kuhusu kuunganisha mifumo hiyo umepita. Hivyo, Serikali itaziita wizara zenye dhamana ya masuala hayo kwa ajili ya kikao cha pamoja kitakacholenga kujadili namna ya kupata suluhisho.
‎
‎Amesisitiza kuwa hatua hiyo inalenga kuweka utaratibu utakaowezesha fursa za ajira na maendeleo ya vijana kukusanywa katika sehemu moja, ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa na kuhakikisha vijana wa Kitanzania wanazifikia fursa hizo kwa urahisi na kwa wakati.
‎

About the author

Alex Sonna