Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), akizungumza wakati akifungua mafunzo ya Siku mbili ya Wahariri wa Vyombo vya Habari na Wamiliki wa Mitandao ya kijamii ya Habari, katika ukumbi wa Hoteli ya Timeless, mjini Morogoro, ambapo aliwataka wanahabari kutumia kalamu zao na weledi wao katika kuongeza uelewa wa umma kuhusu Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi, 2025, kwa kuzingatia takwimu sahihi, kueleza fursa zinazotokana na Sera hiyo, pamoja na namna inavyolenga kuimarisha matumizi bora ya rasilimali za umma.

Kaimu Kamishna wa Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma, Bw. Alex Haraba, akizungumza wakati akimkaribisha Mgeni Rasmi Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb) (hayupo pichani), kufungua mafunzo ya Siku mbili ya Wahariri wa Vyombo vya Habari na Wamiliki wa Mitandao ya kijamii ya Habari kuhusu Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi, 2025, katika ukumbi wa Hoteli ya Timeless, mjini Morogoro.



Baadhi ya Wahariri wa Vyombo vya Habari wakisikiliza hotuba ya Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb) (hayupo pichani), wakati akifungua mafunzo ya Siku mbili ya Wahariri wa Vyombo vya Habari na Wamiliki wa Mitandao ya kijamii ya Habari kuhusu Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi, 2025, katika ukumbi wa Hoteli ya Timeless, mjini Morogoro.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb) (Katikati aliyeketi)), Kaimu Kamishna wa Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma, Bw. Alex Haraba (wa pili kushoto aliyeketi), na maafisa wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha wakiwa katika picha ya pamoja na Wahariri wa Vyombo vya Habari, mara baada ya ufunguzi wa mafunzo ya Siku mbili ya Wahariri hao na Wamiliki wa Mitandao ya kijamii ya Habari kuhusu Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi, 2025, katika ukumbi wa Hoteli ya Timeless, mjini Morogoro.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb) (Katikati aliyeketi), Kaimu Kamishna wa Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma, Bw. Alex Haraba (wa pili kushoto aliyeketi), na maafisa wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha wakiwa katika picha ya pamoja na maafisa wa Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma Wizara ya Fedha, mara baada ya ufunguzi wa mafunzo ya Siku mbili ya Wahariri Vyombo vya Habari na Wamiliki wa Mitandao ya kijamii ya Habari kuhusu Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi, 2025, katika ukumbi wa Hoteli ya Timeless, mjini Morogoro.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Morogoro)
Na. Joseph Mahumi na Ramadhani Kissimba, WF, Morogoro
Serikali imewataka wanahabari kutumia kalamu zao na weledi wao kuongeza uelewa wa umma kuhusu Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi, 2025, kwa kuzingatia takwimu sahihi, kueleza fursa zinazotokana na Sera hiyo, pamoja na namna inavyolenga kuimarisha matumizi bora ya rasilimali za umma.
Wito huo umetolewa na Mhe. Naibu Waziri wa Fedha, Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), wakati akifungua mafunzo ya Siku mbili ya Wahariri wa Vyombo vya Habari na Wamiliki wa Mitandao ya kijamii ya Habari, katika ukumbi wa Hoteli ya Timeless, mjini Morogoro.
Mhe. Munde alisema kuwa vyombo vya habari vina nafasi muhimu katika kujenga uelewa wa wananchi kuhusu sera na namna inavyogusa matumizi ya rasilimali za umma, pamoja na namna mnyororo wa ugavi unavyohusisha hatua mbalimbali, ikiwemo utambuzi na upangaji wa mahitaji, ununuzi, ugomboaji, upokeaji, utunzaji na uhifadhi, matumizi, usambazaji pamoja na uondoshaji wa bidhaa, vifaa na mali.
“Usimamizi wa mnyororo wa ugavi una athari ya moja kwa moja katika namna rasilimali za umma zinavyotumika na namna huduma zinavyowafikia wananchi, hivyo Sera hii ni nyenzo muhimu katika kuimarisha ufanisi, uwajibikaji, uwazi na matumizi yenye tija ya fedha za umma katika shughuli za mnyororo wa ugavi katika Sekta ya Umma” alisema Mhe. Munde
Alisema kuwa utekelezaji wa Sera hiyo unatoa fursa ya kuimarisha ushiriki wa wazalishaji, kampuni na watoa huduma wa ndani katika shughuli za mnyororo wa ugavi, na hatua hizo zinaangalia pia kuongeza matumizi ya bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini, kuendeleza wataalamu wa ndani na kutumia teknolojia katika shughuli mbalimbali za mnyororo wa ugavi.
“Wahariri na Waandishi wa Habari ni kiungo muhimu kati ya Serikali, wadau na wananchi katika kufikisha taarifa hizi za kisera na kitaalamu kwa lugha rahisi na inayoeleweka ndio maana mpo hapa leo kupata uelewa zaidi kuhusu Sera hii” alisema Mhe. Munde.
Aliongeza kuwa jukumu la vyombo vya habari halipaswi kuishia katika kuripoti shughuli za utekelezaji wa Sera, bali pia kufuatilia maendeleo, kubaini changamoto na kuibua maeneo yanayohitaji maboresho kwa kuwa uandishi unaozingatia ukweli na ushahidi unaweza kusaidia kujenga mjadala wa kitaifa kuhusu utekelezaji wa Sera na kuwasaidia wananchi kuelewa matokeo yanayopatikana.
Aidha, Mhe. Munde aliwataka waandishi wa habari kutoa taarifa kuhusu fursa zinazoweza kupatikana kupitia utekelezaji wa Sera hiyo, hususan katika maeneo ya biashara, uzalishaji, teknolojia, ajira na uendelezaji wa uwezo wa ndani kwa kuwa taarifa hizo zitawasaidia wananchi na wadau kutambua nafasi zao katika mnyororo wa ugavi na kutumia fursa zinazojitokeza.
Mhe. Munde aliahidi kuwa Wizara ya Fedha itaendelea kushirikiana na vyombo vya habari kwa kutoa taarifa na ufafanuzi unaohitajika kupitia mamlaka na vyanzo rasmi na mafunzo hayo ni fursa ya kujenga uelewa wa pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya Wizara ya Fedha na vyombo vya habari katika kufikisha taarifa sahihi kwa umma.
“Ninatarajia kuwa baada ya mafunzo haya, mtayatumia maarifa mtakayoyapata kuandaa maudhui yenye taarifa sahihi, yanayoeleweka na yanayozingatia maslahi ya umma” alisema Mhe. Munde
Kwa upande wake, Kaimu Kamishna wa Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma, Bw. Alex Haraba, alisema kuwa Sera hiyo imeweka mwelekeo wa usimamizi wa mnyororo wa ugavi nchini. Katika kutekeleza Sera hiyo, Serikali imeandaa Mkakati wa Utekelezaji wa Sera kwa kipindi cha mwaka 2026–2036, unaoainisha hatua na maeneo ya utekelezaji wa malengo yaliyowekwa.
Bw. Haraba alisema kuwa Utekelezaji wa Sera na Mkakati wake unahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali, wakiwemo waandishi na wahariri wa vyombo vya habari, katika kutoa taarifa na kuelimisha umma kuhusu masuala ya usimamizi wa mnyororo wa ugavi.
“Mafunzo haya yamebeba mada kuu isemayo: “Kuelewa Sera, Kuelimisha Umma na Kufuatilia Utekelezaji wa Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi”, Tunatarajia pia, mafunzo haya yataimarisha uhusiano wa kitaalamu na endelevu kati ya Wizara ya Fedha na vyombo vya habari, hususan katika upatikanaji na matumizi ya taarifa rasmi kuhusu utekelezaji wa Sera” alisema Bw Haraba.
Naye Mwenyekiti wa Wahariri waliohudhuria mafunzo hayo, Bw. Ben Mwang’onda, alisema kuwa, Wizara ya Fedha imekua mstari wa mbele katika kuwajengea uwezo wanahabari mara kwa mara na wanauhakika mafunzo hayo yatasaidia kuongeza maarifa yao katika kuelimisha umma kuhusu masuala ya ununuzi na ugavi.