Picha ni baadhi ya wananchi waliofika kwaajili ya kuwapatia wanyama chanjo kuwanga na magonjwa. Picha na Stephen Noel.
Na Stephen Noel
SERIKALI ya Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma imeitaka Idara ya Mifugo kuongeza kasi ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu chanjo na utunzaji sahihi wa wanyama, hususan mbwa, ili kudhibiti kuenea kwa ugonjwa wa kichaa cha mbwa na kulinda afya za binadamu.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Dkt. Sophia Mfaume Kizigo, kupitia hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Kaimu Mkuu wa Wilaya hiyo, Obert Mwalyego, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kichaa cha Mbwa Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Ilolo, mjini Mpwapwa.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, Mwalyego amesema elimu kwa jamii ni nyenzo muhimu katika kupambana na ugonjwa huo, hivyo ni wajibu wa wataalamu wa mifugo kuendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu njia za kujikinga, umuhimu wa chanjo na namna bora ya kutunza wanyama wao.
Amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuhakikisha mbwa na wanyama wengine wanaohusika wanapatiwa chanjo kwa wakati, pamoja na matibabu yanayostahili, huku wamiliki wakizingatia taratibu za usalama ili kuzuia wanyama hao kusababisha madhara kwa watu.
Amesema ushirikiano kati ya Serikali, wataalamu wa mifugo na wananchi ni muhimu katika kufanikisha juhudi za kudhibiti ugonjwa huo, akieleza kuwa uelewa wa kutosha kuhusu kichaa cha mbwa utasaidia jamii kuchukua hatua za mapema na kupunguza hatari ya maambukizi.
Kwa upande wake, Afisa Mifugo wa Wilaya ya Mpwapwa, Dkt. Emanuel Lyimo, amesema maadhimisho hayo yametumika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu dhana ya Afya Moja (One Health), inayosisitiza uhusiano uliopo kati ya afya ya binadamu, wanyama na mazingira.
Dkt. Lyimo amesema dhana hiyo inahitaji wadau wa sekta hizo kushirikiana katika kuzuia na kudhibiti magonjwa yanayoweza kuenezwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu, yakiwemo ya kichaa cha mbwa. Ameongeza kuwa wananchi wameelimishwa kuhusu utunzaji wa mazingira na hatua za kujikinga dhidi ya ugonjwa huo.
Amesisitiza kuwa kuimarisha uelewa wa jamii, kuongeza wigo wa utoaji wa chanjo na kuwajibika katika utunzaji wa wanyama ni hatua muhimu katika kulinda afya za wananchi na kujenga mazingira salama kwa binadamu na wanyama.
Maadhimisho ya Siku ya Kichaa cha Mbwa Duniani hulenga kuongeza uelewa kuhusu madhara ya ugonjwa huo na kuhamasisha juhudi za pamoja za kuudhibiti kupitia chanjo, elimu kwa jamii na uwajibikaji wa wamiliki wa wanyama.