Wakulima wa kahawa Tanzania wanaonufaika na programu za Taasisi ya Hanns R. Neumann Stiftung (HRNS) wameondolewa hofu kufuatia mabadiliko ya uongozi katika taasisi hiyo, huku uongozi ukisisitiza kuwa mabadiliko hayo hayataleta mabadiliko katika dhamira yake ya kusaidia wakulima, bali yataimarisha zaidi kazi hiyo.
Kuanzia Oktoba 1, 2026, Michael R. Neumann ataachia nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya HRNS baada ya zaidi ya miongo miwili, na nafasi hiyo kuchukuliwa na Dkt. Nina Smidt, mtendaji mwenye uzoefu wa kimataifa katika uendeshaji wa taasisi za kijamii, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji na Msemaji wa Bodi ya Siemens Stiftung.
HRNS, yenye makao yake nchini Ujerumani na inayosaidia jamii zinazolima kahawa, imekuwa ikifanya kazi na wakulima Tanzania tangu mwaka 2006. Mabadiliko hayo yanakuja wakati wakulima wakikabiliwa na changamoto zinazoongezeka, zikiwemo mabadiliko ya tabianchi, kupanda kwa gharama za uzalishaji na haja ya fursa endelevu zaidi za kiuchumi.
Meneja wa HRNS Tanzania, Morgan Mkonyi, amesema mabadiliko hayo yatajengwa juu ya kazi iliyofanywa na taasisi hiyo badala ya kubadili msingi wa dhamira yake.
“Mchango wa Michael R. Neumann katika ukuaji na maendeleo ya HRNS umeweka msingi imara ambao tunaweza kuendelea kuujengea. Tunapomkaribisha Dkt. Nina Smidt kama Mwenyekiti mpya, tunaona mabadiliko haya si kama kuachana na dhamira yetu, bali kama fursa ya kuiimarisha na kuisogeza mbele zaidi,” alisema.
Mkonyi alisema HRNS imepanua wigo wa kazi zake kutoka kuongeza uzalishaji wa kahawa pekee hadi kushughulikia mazingira mapana yanayoamua ustawi endelevu wa wakulima na familia zao.
Kwa sasa, programu za HRNS zinajumuisha kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi, agroforestry, ulinzi wa mazingira, fursa za kiuchumi kwa vijana na kuimarisha mashirika ya wakulima, sambamba na juhudi za kuongeza uzalishaji wa kahawa.
“Kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi pamoja na agroforestry kinaweza kuwasaidia wakulima kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa huku wakilinda rutuba ya udongo na vyanzo vya maji,” alisema Mkonyi.
Alisema kuimarika kwa mashirika ya wakulima kunaweza kuongeza uwezo wao wa kupata huduma, maarifa na masoko, huku programu za vijana zikilenga kujenga fursa mpya za kiuchumi kwa kizazi kijacho. HRNS pia imekuwa ikichunguza miradi ya kaboni inayounganisha uzalishaji wa kilimo na uhifadhi wa mazingira.
Kwa mujibu wa Mkonyi, mafanikio ya kazi hiyo yanapaswa kupimwa kwa athari zake kwa watu na jamii.
“Kwetu sisi Tanzania, mafanikio ya HRNS hatimaye yanaonekana katika maisha ya familia za wakulima wadogo, vijana na jamii tunazofanya nazo kazi,” alisema.
Aliongeza kuwa mabadiliko ya kudumu katika jamii za vijijini yanahitaji muda, ushirikiano na suluhisho zinazoendana na mazingira ya eneo husika.
Neumann, aliyeanzisha HRNS pamoja na familia yake mwaka 2005, amesimamia upanuzi wa taasisi hiyo kutoka mipango iliyolenga zaidi kahawa hadi kuwa taasisi pana ya maendeleo ya kimataifa.
Akieleza uamuzi wake wa kukabidhi nafasi hiyo, alisema:“Baada ya zaidi ya miaka 20, wakati umefika kwangu kukabidhi nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini kwa kizazi kijacho. Nafanya hivyo kwa kujiamini kwa sababu Hanns R. Neumann Stiftung ina msingi imara na iko tayari kuendelea kukua na kujiendeleza.”
Dkt. Smidt, ambaye ana uzoefu mkubwa katika ushirikiano wa kimataifa na maendeleo ya kimkakati ya mashirika yasiyo ya kiserikali, amesema uhusiano wake na HRNS umejengwa juu ya maadili yanayofanana na dhamira ya kuleta matokeo ya kudumu kupitia ushirikiano.
Kwa wakulima wa kahawa Tanzania, mafanikio ya uongozi mpya hatimaye yatapimwa si kwa mabadiliko yaliyofanyika katika uongozi wa taasisi, bali kwa matokeo yatakayoonekana katika vijiji vinavyolima kahawa—ikiwemo mashamba yenye uwezo mkubwa wa kustahimili changamoto, kuboreka kwa maisha ya kaya, kuimarika kwa mashirika ya wakulima, fursa zaidi kwa vijana na ulinzi bora wa maliasili.
Baada ya miaka 20 ya HRNS nchini Tanzania, mabadiliko haya yanafungua awamu mpya ya kuendeleza uzoefu, ushirikiano na rasilimali zilizojengwa, huku wakulima wakitarajia maboresho makubwa zaidi, yanayopimika na yenye kudumu katika maisha ya familia zinazotegemea kahawa.

Kuanzia Oktoba 1, 2026, Michael R. Neumann (Kulia) ataachia nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya HRNS baada ya zaidi ya miongo miwili, na nafasi hiyo kuchukuliwa na Dkt. Nina Smidt, (kushoto) mtendaji mwenye uzoefu wa kimataifa katika uendeshaji wa taasisi za kijamii, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji na Msemaji wa Bodi ya Siemens Stiftung.