Featured Kitaifa

USHIRIKIANO NI MUHIMU KATIKA MAGEUZI YA KIDIJITALI: KITALI

Written by Alex Sonna

OWM-TAMISEMI, Arusha

Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Bw. Erick Kitali, amesema mafanikio ya mageuzi ya kidijitali nchini yanahitaji ushirikiano wa taasisi mbalimbali, uongozi wenye maono na kuwashirikisha wataalamu sahihi katika kufanya maamuzi.

Bw. Kitali ameyasema hayo leo Septemba 10, 2026 jijini Arusha wakati wa mdahalo kuhusu kuimarisha huduma za afya ya msingi kupitia miundombinu ya umma ya kidijitali na safari ya Tanzania ya kuwalipa wahudumu wa afya ya jamii kwa njia za kidijitali.

Amesema ni muhimu Serikali kuhakikisha mifumo mbalimbali inaunganishwa ili kuwezesha upatikanaji wa taarifa kwa wakati na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Tunapaswa kuzungumzia ushirikiano na muunganiko wa mifumo. hakikisheni watu sahihi wanakuwepo kwenye meza ya maamuzi,” amesema.

Bw. Kitali amesema Tanzania imejikita pia katika kutumia wataalamu wa ndani kubuni, kuendeleza na kusimamia mifumo ya kidijitali inayotumika katika huduma za afya, ikiwemo usajili, malipo na utoaji wa taarifa.

Amesema Serikali imeandaa Mpango Elekezi (Blueprint) wa matumizi ya teknolojia katika huduma za wahudumu wa afya ya jamii, ukiwemo mpango wa kuanzisha Dashibodi ya Pamoja itakayounganisha taarifa kutoka mifumo mbalimbali.

Kwa mujibu wa Bw. Kitali, amesema dashibodi hiyo itasaidia kufuatilia huduma na malipo kuanzia ngazi ya jamii hadi taifa, pamoja na kubaini kwa haraka changamoto kama ucheleweshaji wa malipo.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kufanya tafiti na ufuatiliaji wa utekelezaji ili kubaini changamoto mapema na kuchukua hatua kwa wakati.

Amesema ushirikiano wa taasisi, matumizi ya wataalamu wa ndani na mifumo iliyounganishwa ni msingi muhimu wa kuboresha huduma za afya ya msingi na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa wakati.

About the author

Alex Sonna