Featured Kitaifa

HAKUNA MTOTO ATAACHWA

Written by Alex Sonna

 

Serikali imeweka mkazo katika kutafuta suluhisho la changamoto ya wanafunzi kuacha shule, hususan wavulana, baada ya kubainika kuwa ongezeko la utoro linaweza kuwa kikwazo katika utekelezaji wa mageuzi ya elimu nchini.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema hayo Septemba 03, 2026, Jiji Dodoma alipokutana na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Elke Wisch.

Prof. Mkenda amebainisha kuwa pamoja na juhudi zinazofanyika kuboresha elimu, changamoto ya watoto kuacha shule inahitaji juhudi za pamoja, kwani makadirio ya serikali ya wanafunzi watakaoendelea na elimu yanaweza kuathiriwa iwapo tatizo hilo halitadhibitiwa.

Amesema serikali inaendelea kuweka mikakati ya kuzuia utoro, ikiwemo kuimarisha utekelezaji wa mwongozo wa wanafunzi waliokatisha masomo kurejea shule na kushughulikia changamoto zinazowakabili watoto hao katika maeneo mbalimbali.

Prof. Mkenda amesisitiza kuwa utekelezaji wa mageuzi ya elimu hauishii katika kuandaa sera na mipango pekee, bali unahitaji ushirikiano wa karibu na wadau katika kutatua changamoto halisi zinazowazuia watoto kuendelea na masomo.

Aidha, ameiomba UNICEF kuendelea kushirikiana na serikali katika kupunguza utoro, kusaidia wanafunzi waliokatisha masomo kurejea shuleni na kuimarisha fursa za watoto kupata elimu.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Carolyne Nombo, amesema kuwa serikali inaendelea kuimarisha Mafunzo Endelevu ya Kitaaluma kwa Walimu ili kuwa na mbinu mpya za ufundishaji na zinazoshirikisha wanafunzi kikamilifu katika mchakato wa ujifunzaji.

Mwakilishi wa UNICEF, Elke Wisch, ameipongeza seikali ya Tanzania kwa hatua kubwa inayopiga katika utekelezaji wamageuzi ya sekta ya elimu, akisisitiza kuwa mageuzi hayo ni msingi wa kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kuandaa kizazi kitakachoweza kuendesha uchumi wa kisasa.

About the author

Alex Sonna