Featured Kitaifa

MAKAMU WA RAIS AAGIZA SULUHU YA HARAKA BEI YA SARUJI

Written by Alex Sonna

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi akihutubia wakati wa hafla ya utoaji tuzo za 19 za Rais za Wazalishaji Bora Viwandani (PYMA), zilizofanyika katika Ukumbi wa Super Dome, Masaki Jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, ameiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na wazalishaji wa saruji nchini kutafuta suluhu ya haraka ya kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo ili wananchi waweze kuipata kwa gharama nafuu.

Ndejembi ametoa agizo hilo  jijini Dar es Salaam wakati akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika hafla ya utoaji wa Tuzo za 19 za Rais kwa Wazalishaji Bora Viwandani iliyofanyika katika Ukumbi wa Super Dome, Masaki.

Alisema maono ya Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa muhimu kwa bei inayokidhi uwezo wao, hivyo kuna umuhimu wa kuoanisha uzalishaji wa malighafi zinazotumika katika uzalishaji wa saruji ili kuongeza upatikanaji na kupunguza gharama.

Aidha, Makamu wa Rais aliitaka Serikali kufanya tathmini ya ukuaji wa sekta ya viwanda nchini ili kubaini iwapo kasi hiyo inaendana na uwezo wa viwanda vya ndani kushindana katika masoko ya kikanda, Afrika na kimataifa.

Alisema Serikali itaendelea kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wafanyabiashara wanaoingiza nchini bidhaa bandia na bidhaa zinazoingia kinyume cha taratibu, akieleza kuwa vitendo hivyo vinakwepa kodi na tozo, kuathiri viwanda vya ndani na kupunguza ushindani wa bidhaa zinazozalishwa nchini.

Ndejembi pia aliwataka wazalishaji kuongeza uchakataji wa malighafi ndani ya nchi na kuongeza thamani ya bidhaa kabla ya kuziuza, akisema hatua hiyo itasaidia kuongeza ajira, mapato ya Serikali na kukuza uchumi.

Vilevile, aliiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara kuhakiki takwimu za idadi ya viwanda vilivyopo nchini ili kuweka mikakati ya kuongeza ushiriki wa wazalishaji katika Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), hatua ambayo alisema itasaidia kuwepo kwa chombo madhubuti cha kuwawakilisha wazalishaji.

Alisema sekta ya viwanda ni muhimili muhimu wa uchumi kutokana na nafasi yake katika kuongeza thamani ya malighafi, kutoa ajira, kuongeza mapato ya Serikali na kuingiza fedha za kigeni. Aliongeza kuwa sekta hiyo pia ina mchango katika kukuza sayansi na teknolojia, ubunifu na uvumbuzi.

Ndejembi alisema Tanzania ina fursa kubwa ya kukuza viwanda kutokana na wingi wa rasilimali, ikiwamo misitu na madini, hivyo kuna haja ya kuimarisha uhusiano kati ya sekta ya viwanda na sekta nyingine ili kuongeza tija na kasi ya maendeleo.

Alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kushirikiana kwa karibu na sekta binafsi katika kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na kuharakisha maendeleo ya Taifa.

Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, alisema wizara hiyo imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuimarisha sekta ya viwanda na kuongeza mchango wake katika pato la Taifa.

Kapinga alisema wizara imekamilisha maandalizi ya Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda ya mwaka 2025 pamoja na Sera ya Maendeleo ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya mwaka 2003, Toleo la 2025, ambazo zinalenga kwenda sambamba na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Naye Mwenyekiti wa CTI, Hussein Suphian Ally, aliipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali zinazolenga kuimarisha mazingira ya uwekezaji na kuongeza ushindani wa viwanda vya ndani.

Alisema uwekezaji katika miradi ya kimkakati, ikiwamo Reli ya Kisasa (SGR), bandari, barabara, nishati na miundombinu mingine ya kiuchumi, umeendelea kupunguza gharama za usafirishaji, kurahisisha biashara na kusaidia bidhaa zinazozalishwa nchini kufikia masoko ya ndani, kikanda na kimataifa.

Katika hafla hiyo, Rais Samia alitunukiwa tuzo ya heshima kwa kutambua mchango wake katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na maendeleo ya sekta ya viwanda nchini.

Hafla hiyo iliwakutanisha wazalishaji wakubwa, wa kati na wadogo, wafanyabiashara pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya viwanda na biashara, huku tuzo hizo zikitajwa kuwa jukwaa muhimu la kuhamasisha ubora, ubunifu, uwekezaji, matumizi ya teknolojia na uzalishaji endelevu nchini.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi akisalimiana na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga, wakati akiwasili katika Ukumbi wa Super Dome, Masaki Jijini Dar es Salaam, kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika utoaji tuzo za 19 za Rais za Wazalishaji Bora Viwandani (PYMA).

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi akisalimiana na Viongozi mbalimbali, wakati akiwasili katika Ukumbi wa Super Dome, Masaki Jijini Dar es Salaam, kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika utoaji tuzo za 19 za Rais za Wazalishaji Bora Viwandani (PYMA).

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi akishiriki usiku wa tuzo za 19 za Rais za Wazalishaji Bora Viwandani (PYMA), wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika hafla hiyo, iliyofanyika katika Ukumbi wa Super Dome, Masaki Jijini Dar es Salaam.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi akihutubia wakati wa hafla ya utoaji tuzo za 19 za Rais za Wazalishaji Bora Viwandani (PYMA), zilizofanyika katika Ukumbi wa Super Dome, Masaki Jijini Dar es Salaam.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi akikabidhi tuzo kwa mshindi wa jumla wa tuzo za 19 za Rais za Wazalishaji Bora Viwandani (PYMA), ambayo ni kampuni ya Silafrica Tanzania LTD. katika hafla iliyofanyika Ukumbi wa Super Dome, Masaki Jijini Dar es Salaam.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi akikabidhiwa tuzo iliyotolewa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua mchango wake katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na viwanda nchini wakati wa hafla ya utoaji tuzo za 19 za Rais za Wazalishaji Bora Viwandani (PYMA), zilizofanyika katika Ukumbi wa Super Dome, Masaki Jijini Dar es Salaam. (anayekabidhi ni Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga, kushoto ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) Hussein Suphian Ally)

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi akiwa katika picha ya pamoja na washindi wa tuzo za 19 za Rais za Wazalishaji Bora Viwandani (PYMA), mara baada ya kuhitimisha utoaji wa tuzo hizo katika hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Super Dome, Masaki Jijini Dar es Salaam.

About the author

Alex Sonna