Featured Kitaifa

BALOZI OMAR: UWEZO WA KITAALUMA UAMBATANE NA MAADILI

Written by Alex Sonna

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akiagana na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Wahasibu, Wakaguzi na Washauri Elekezi wa Kodi Zanzibar (ZIAAT), CPA Ame Burhan Shadhil, mara baada ya kikao chao kilichofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Saalam, ambapo walijadili namna Taasisi hiyo itahakikisha inajenga uwezo wa kitaaluma kwa Wahasibu, Wakaguzi na Washauri Elekezi wa Kodi unaoambatana na maadili, ili taaluma hizo ziweze kuwa na tija kwa jamii.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akizungumza wakati wa kikao chake na ujumbe wa Taasisi ya Wahasibu, Wakaguzi na Washauri Elekezi wa Kodi Zanzibar (ZIAAT), ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wake, CPA Ame Burhan Shadhil, uliofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Saalam, ambapo walijadili namna Taasisi hiyo itahakikisha inajenga uwezo wa kitaaluma kwa Wahasibu, Wakaguzi na Washauri Elekezi wa Kodi unaoambatana na maadili, ili taaluma hizo ziweze kuwa na tija kwa jamii.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akiongoza kikao chake na ujumbe wa Taasisi ya Wahasibu, Wakaguzi na Washauri Elekezi wa Kodi Zanzibar (ZIAAT), ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wake, CPA Ame Burhan Shadhil, uliofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Saalam, ambapo walijadili namna Taasisi hiyo itahakikisha inajenga uwezo wa kitaaluma kwa Wahasibu, Wakaguzi na Washauri Elekezi wa Kodi unaoambatana na maadili, ili taaluma hizo ziweze kuwa na tija kwa jamii.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dar es Salaam)

Na Peter Haule na Joseph Mahumi, WF, Dar es Salaam

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), ametoa rai kwa Taasisi ya Wahasibu, Wakaguzi na Washauri Elekezi wa Kodi Zanzibar (ZIAAT) kuhakikisha kuwa inajenga uwezo wa kitaaluma unaoambatana na maadili, ili taaluma hizo ziwe na tija kwa jamii.

Ametoa rai hiyo alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa ZIAAT ulioongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, CPA Ame Burhan Shadhil, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.

Mhe. Balozi Omar alisema kuwa Taifa linahitaji wataalamu wenye uwezo na weledi katika taaluma zao, lakini pia wenye maadili yanayoendana na elimu, utaalamu na ujuzi walioupata, akisisitiza kuwa maadili ni msingi muhimu katika kuhakikisha taaluma zinakuwa na mchango chanya katika maendeleo ya Taifa kwa sasa na kwa vizazi vijavyo.

“Tumebadilishana mawazo kuhusu namna ya kusimamia taaluma na namna ambavyo ZIAAT inaweza kuendelea kushirikiana na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) ili kuimarika zaidi,” alisema Mhe. Balozi Omar.

Alisema kuwa ni muhimu ZIAAT kuendelea kushirikiana na taasisi zinazohusika na usimamizi wa taaluma hizo, ikiwemo NBAA, ili kupata ithibati (accreditation) na usajili unaotambulika katika taasisi mbalimbali za kitaaluma ndani na nje ya Tanzania.

“NBAA imekuwa ikishirikiana na ZIAAT katika kuwawezesha kupata usajili katika baadhi ya taasisi ndani ya Bara la Afrika, na ni muhimu ushirikiano huo ukaendelea,” alisema.

Aidha, Mhe. Balozi Omar alisema kuwa kuna ushirikiano mkubwa kati ya Mhasibu Mkuu wa Serikali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhasibu Mkuu wa Serikali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), hususan katika ujenzi wa uwezo wa wataalamu na uimarishaji wa mifumo ya kitaaluma.

Alisema kuwa ushirikiano huo ni muhimu kwa kuwa ZIAAT inashughulikia maeneo mbalimbali ya taaluma, yakiwemo uhasibu, ukaguzi wa hesabu, ushauri wa masuala ya kodi pamoja na taaluma ya manunuzi (procurement).

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Wahasibu, Wakaguzi na Washauri Elekezi wa Kodi Zanzibar (ZIAAT), CPA Ame Burhan Shadhil, alimshukuru Mhe. Balozi Omar kwa kuonesha utayari wa kushirikiana na taasisi hiyo katika kuongeza ubora na weledi wa taaluma.

Alisema kuwa ZIAAT ni taasisi changa, lakini imeendelea kushirikiana vizuri na NBAA kupitia Mkataba wa Makubaliano (MoU), unaowezesha taasisi hizo kushirikiana katika utoaji wa elimu na uendeshaji wa semina za Maendeleo Endelevu ya Kitaaluma (CPD).

“Pamoja na kwamba taasisi yetu ni changa, tumekuwa na ushirikiano mzuri na NBAA kupitia MoU tuliyoingia. Kupitia ushirikiano huo, tumekuwa tukishirikiana katika utoaji wa elimu na kuendesha semina za CPD, ambapo kwa sasa tunafanya semina mbili kila mwaka,” alisema CPA Shadhil.

Aidha, alisema ZIAAT inatoa kozi ya Utaalamu wa Kodi (Professional Tax) inayowalenga wataalamu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, hivyo akatoa wito kwa wataalamu wa masuala ya kodi kutumia fursa hiyo kujiendeleza kitaaluma.

CPA Shadhil alisema Tanzania ina uhitaji mkubwa wa wataalamu wenye ubobezi katika masuala ya kodi, hivyo ni muhimu wataalamu kutumia fursa zilizopo ili kuimarisha taaluma hiyo na hatimaye kuwa na wataalamu bora wa Kodi nchini.

Alisema kuwa ushirikiano kati ya taasisi za kitaaluma ni muhimu katika kujenga uwezo, kuimarisha weledi na kuhakikisha kuwa wataalamu wanakuwa na elimu, ujuzi na maadili yanayokidhi mahitaji ya Taifa.

Kikao hicho klihudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya, Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA. Leonard Mkude, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA Prof. Siasa Mzenzi, Kaimu Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali, Mhandisi Kenneth Nindie na maafisa wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha na ZIAAT.

About the author

Alex Sonna