Featured Kitaifa

SERIKALI, KPMG KUIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA MABORESHO YA MFUMO WA KODI

Written by Alex Sonna

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akizungumza wakati wa kikao chake na Uongozi wa Kampuni ya Kimataifa ya Ukaguzi na Ushauri wa Kitaalamu ya KPMG East Africa, ukiongozwa na Mkurugenzi Msimamizi wa Kampuni hiyo, Bw. Alexander Njombe (hayupo pichani), katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam, ambapo walijadili kuendelea kuimarisha ushirikiano hususan katika masuala ya sera za kodi, usimamizi wa mapato na mageuzi ya mfumo wa kodi, ili kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato na kuwezesha utekelezaji wa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akiongoza kikao chake na Uongozi wa Kampuni ya Kimataifa ya Ukaguzi na Ushauri wa Kitaalamu ya KPMG East Africa, ukiongozwa na Mkurugenzi Msimamizi wa Kampuni hiyo, Bw. Alexander Njombe, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam, ambapo walijadili kuendelea kuimarisha ushirikiano hususan katika masuala ya sera za kodi, usimamizi wa mapato na mageuzi ya mfumo wa kodi, ili kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato na kuwezesha utekelezaji wa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (wa tatu kulia), Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya (wa pili kushoto), Mkurugenzi Msimamizi wa Kampuni ya Kimataifa ya Ukaguzi na Ushauri wa Kitaalamu ya KPMG East Africa, Bw. Alexander Njombe (wa pili kulia), Mshirika wa Masuala ya Kodi wa KPMG (Tax Partner), Bi. Fabiola Ssebuyoya (wa tatu kushoto), na Mshirika wa Huduma za Uhakiki na Ukaguzi (Assurance Partner), Bw. Adolph Boyo (kulia), wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kikao chao kilichofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam, ambapo walijadili kuendelea kuimarisha ushirikiano hususan katika masuala ya sera za kodi, usimamizi wa mapato na mageuzi ya mfumo wa kodi, ili kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato na kuwezesha utekelezaji wa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dar es Salaam)

Na. Joseph Mahumi na Peter Haule, WF, Dar es Salaam

Serikali imesema itaendelea kuimarisha ushirikiano na Kampuni ya Kimataifa ya Ukaguzi na Ushauri wa Kitaalamu ya KPMG, hususan katika masuala ya sera za kodi, usimamizi wa mapato na mageuzi ya mfumo wa kodi, ili kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato na kuwezesha utekelezaji wa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), alipokutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa KPMG East Africa, ukiongozwa na Mkurugenzi Msimamizi wa Kampuni hiyo, Bw. Alexander Njombe, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.

Alisema kuwa Serikali inathamini mchango wa kampuni hiyo kupitia huduma za ushauri wa kitaalamu na kisera katika kusaidia Serikali kufanya maboresho mbalimbali yenye tija kwa uchumi wa Taifa.

“Serikali inafurahia ushauri tunaoupata kutoka KPMG, hasa katika masuala ya sera, tunathamini ushirikiano huu kwa sababu unatupa fursa ya kupata mtazamo mpana na ushahidi unaoweza kutusaidia kuboresha maamuzi yetu,” alisema Mhe. Balozi Omar.

Mhe. Balozi Omar alisema ushirikiano kati ya Serikali na KPMG umejikita katika maeneo mbalimbali, ikiwemo mazungumzo ya kisera, ushauri wa kitaalamu na kiufundi, pamoja na masuala yanayohusu maboresho ya mfumo wa kodi, na Serikali imekuwa ikinufaika na ushauri unaotolewa na wataalamu wa KPMG, ambao mara nyingi hujikita katika ushahidi na takwimu, jambo linalosaidia Serikali kufanya maamuzi yanayozingatia uhalisia wa mazingira ya kiuchumi.

Aidha alisema Serikali haiwezi kufanya mageuzi ya mfumo wa kodi kwa kujifungia ndani ya taasisi zake pekee, bali inahitaji pia maoni na uzoefu kutoka kwa wataalamu wa sekta binafsi na taasisi zenye uzoefu katika nchi mbalimbali, na uwepo wa KPMG nchini Tanzania na nchi nyingine za ukanda wa Afrika unatoa fursa ya kufanya ulinganisho wa mifumo ya kodi na kujifunza uzoefu wa nchi nyingine, hatua ambayo inaweza kusaidia kuendelea kuboresha mazingira ya kodi nchini.

Aliongeza kuwa katika kuendeleza ushirikiano huo, Serikali imeainisha maeneo mbalimbali ambayo inaweza kushirikiana na KPMG, ambayo ni muhimu katika kipindi ambacho Tanzania imeanza kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, na yataibadilisha Tanzania kuwa nchi yenye uchumi shindani, unaozalisha fursa na kuboresha maisha ya wananchi.

“Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni ya wote, hatuwezi kusema Serikali ifanye kila kitu peke yake, wakati sekta binafsi ndiyo inayofanya sehemu kubwa ya shughuli za kiuchumi,  tunahitaji kukaa pamoja, kushauriana na kujenga mambo yatakayosaidia Taifa kufikia malengo tuliyojiwekea,” alisema Mhe. Balozi Omar.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msimamizi wa Kampuni ya Kimataifa ya Ukaguzi na Ushauri wa Kitaalamu ya KPMG East Africa, Bw. Alexander Njombe, alisema kuwa KPMG iko tayari kuendelea kutumia mtandao wake wa kikanda na kimataifa, pamoja na utaalamu wa wataalamu wake katika sekta mbalimbali, kusaidia Serikali ya Tanzania kupata maarifa na uzoefu unaoweza kuchochea uwekezaji na maendeleo katika mikoa na sekta mbalimbali nchini.

Alisema kuwa kupitia uwepo wa KPMG katika nchi nyingi za Afrika na duniani, Serikali inaweza kunufaika na uzoefu na mbinu bora zinazotekelezwa katika maeneo mengine, hususan katika matumizi ya teknolojia na Akili Unde(AI), ufanyaji wa maamuzi unaozingatia takwimu, ufanisi wa kiutendaji pamoja na utaalamu mahsusi katika sekta kama nishati na maliasili, jambo ambalo linaweza kusaidia kuongeza ufanisi wa sera na uwekezaji na kuchangia utekelezaji wa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya, Mshirika wa Masuala ya Kodi wa KPMG (Tax Partner), Bi. Fabiola Ssebuyoya, Mshirika wa Huduma za Uhakiki na Ukaguzi (Assurance Partner), Bw. Adolph Boyo na maafisa wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha.

About the author

Alex Sonna