Mkurugenzi wa Bayer Tanzania Sango Mwinyi ( mwenye namba 8) akiwa kwa picha ya pamoja na wadau wa mbegu kutoka Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) na wakulima wa mkoa wa morogoro, pamoja na wauza pembejeo kutoka Morogoro wakati wa uzinduzi wa kampeni yake ya kitaifa ya uhamasishaji kwa wakulima ili kuwaongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kutumia na kuhakiki mbegu halisi kabla ya msimu wa kilimo inayofahamika kama “DEKALB Mafanikio Shambani’’. Uzinduzi huo umefanyika katikati ya wiki hii.
…..
Wakulima wa mahindi nchini wametahadharishwa dhidi ya kutumia mbegu zisizothibitishwa ubora, wakihimizwa kuhakikisha mbegu wanazonunua zimehakikiwa kabla ya kuzipanda ili kuepuka hasara na kupunguza hatari ya kupata mavuno duni.
Tahadhari hiyo imetolewa na Bayer Tanzania kupitia kampeni yake ya kitaifa ya uhamasishaji kwa wakulima inayolenga kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kutumia na kuhakiki mbegu halisi kabla ya msimu wa kilimo.
Kampeni hiyo inayojulikana kama “DEKALB Mafanikio Shambani” imeendelea Mkoani Morogoro baada ya kuzinduliwa mapema mwezi huu, ikiwa na lengo la kuwafikia wakulima katika maeneo mbalimbali nchini na kuwapatia elimu kuhusu mbegu bora na suluhisho za kisasa za kilimo.
Mkurugenzi wa Bayer Tanzania, Sango Mwinyi, alisema matumizi ya mbegu zisizothibitishwa yanaweza kuwaweka wakulima katika hatari ya kupoteza uwekezaji wao, hasa katika kipindi ambacho kilimo kinakabiliwa na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi na hali ya hewa isiyotabirika.
“Wakulima wanapaswa kuwa makini wanaponunua mbegu na kuhakikisha wanazihakiki kabla ya kupanda. Bila kupata taarifa sahihi na kufanya uhakiki, wakulima wanaweza kununua na kupanda mbegu zisizo sahihi na hatimaye kupoteza sehemu kubwa ya uwekezaji wao kutokana na mavuno duni,” alisema Mwinyi.
Alisema wakulima wadogo, ambao ni sehemu muhimu ya mfumo wa chakula nchini, wanahitaji kupata taarifa sahihi ili kufanya maamuzi sahihi kuhusu pembejeo wanazotumia katika mashamba yao.
Kwa mujibu wa Mwinyi, mabadiliko ya tabianchi yameongeza umuhimu wa wakulima kutumia mbegu zilizothibitishwa na zinazofaa kwa mazingira husika ili kuongeza uwezekano wa kupata mavuno yenye uhakika.
“Wakulima wadogo wanaendelea kukabiliwa na changamoto kubwa zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi na hali ya hewa isiyotabirika. Katika mazingira haya, matumizi ya mbegu zilizothibitishwa ni muhimu zaidi kwa sababu zinawasaidia wakulima kuongeza tija na kujenga ustahimilivu wa kilimo,” alisema.
Kupitia kampeni hiyo, Bayer inahamasisha matumizi ya aina tano za mbegu chotara za mahindi za DEKALB, ambazo zimetengenezwa kwa kuzingatia maeneo mbalimbali ya kilimo nchini, ikiwemo maeneo yenye mvua chache na yale yenye uwezo mkubwa wa uzalishaji.
Mbali na elimu kwa wakulima, kampeni hiyo pia imeambatana na promosheni yenye zawadi mbalimbali kwa wakulima wanaonunua na kuhakiki mbegu halisi za DEKALB. Zawadi hizo ni pamoja na pampu za kunyunyizia dawa za mgongoni, simu janja, mashine za kupandia mahindi zinazoendeshwa kwa mkono, pikipiki, mifumo ya umeme wa jua na mashine za kumenya mahindi.
Aidha, wakulima wawili watakaobahatika watajishindia gari aina ya Toyota pick-up kila mmoja mwishoni mwa kampeni hiyo.
Ili kushiriki, wakulima wanatakiwa kununua mbegu za DEKALB kutoka kwa wauzaji wa pembejeo walioidhinishwa, kisha kukwangua kibandiko cha TOSCI kilichopo kwenye kifungashio ili kupata namba ya kipekee ya uhakiki.
Baada ya hapo, mkulima anatakiwa kupiga *148*52# na kuingiza namba ya uhakiki yenye tarakimu 12. Baada ya mbegu kuthibitishwa, mkulima atapokea ujumbe mfupi wa uthibitisho na kuingizwa moja kwa moja kwenye droo ya promosheni.
Mwinyi, ambaye pia ni Kiongozi wa Biashara ya Sayansi ya Mazao nchini Tanzania katika Bayer East Africa, alisema kampeni hiyo inalenga zaidi kumwezesha mkulima kufanya uamuzi sahihi kabla ya kuwekeza katika uzalishaji.
“Kila msimu wa kilimo ni uwekezaji mkubwa kwa kaya za wakulima. Hivyo, kuhakikisha mbegu ni halisi na zenye ubora kabla ya kupanda ni hatua muhimu ya kulinda uwekezaji huo. Tunawahamasisha wakulima wasinunue mbegu kwa kuangalia bei pekee, bali wahakikishe pia uhalali na ubora wake kabla ya kupanda,” alisisitiza.
Kampeni ya DEKALB Mafanikio Shambani inatarajiwa kudumu kwa miezi minne, ikilenga kuongeza uelewa miongoni mwa wakulima kuhusu umuhimu wa kutumia mbegu zilizothibitishwa, kuongeza tija ya kilimo na kuchangia katika kuimarisha usalama wa chakula nchini.