BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imeikabidhi Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) jukumu la kusimamia mchakato wa maombi na uteuzi wa wanufaika wa Mfuko wa Udhamini wa Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (Mwalimu Nyerere Memorial Scholarship Fund), hatua inayolenga kuongeza uwazi, usawa na ufanisi katika utoaji wa ufadhili kwa wanufaika wa elimu ya juu nchini.
Uamuzi huo umeanza kutumika katika udahili wa mwaka wa masomo 2026/27 baada ya Bodi ya Usimamizi wa Mfuko huo kuridhia kutumia mifumo ya HESLB katika mchakato wa kutangaza, kupokea na kuchakata maombi ya wanafunzi wanaostahili kupata ufadhili.
Hayo yamesemwa leo Agosti 28,2026 jijini Dar es Salaam na Gavana wa BoT, Bw. Emmanuel Tutuba wakati akizindua Mwongozo Mpya wa Utoaji Ufadhili kwa Wanafunzi wanaonufaika na Mfuko wa Udhamini wa Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Gavana Tutuba amesema, uamuzi huo ulifikiwa na Bodi ya Mfuko katika kikao chake kilichofanyika Mei,mwaka huu, baada ya kubaini umuhimu wa kutumia mifumo iliyopo serikalini ili kurahisisha mchakato wa kuwapata wanafunzi wenye sifa.
“Tumekubaliana sasa kutumia mifumo inayoratibiwa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu. Mfumo huo una uwezo wa kutumia taarifa za ufaulu kutoka Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), hivyo kutuwezesha kupata wanafunzi wenye sifa kwa utaratibu wenye ufanisi zaidi,” amesema Gavana Tutuba.
Amesema,mabadiliko hayo yanaendana na msisitizo wa Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu umuhimu wa mifumo ya Serikali kusomana ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Gavana huyo, badala ya kuendelea na utaratibu wa kutangaza nafasi na kusubiri maombi, HESLB itaweza kutumia mifumo yake iliyopo kuchakata taarifa za wanafunzi na kubaini wanaokidhi vigezo vya ufadhili.
“Kwa kuwa mfumo wa Bodi ya Mikopo tayari unachakata taarifa za wanafunzi na kubaini wanaostahili kupata mikopo, tumeona ni jambo jema kutumia utaratibu huo huo katika kupata wanufaika wa Mfuko wa Mwalimu Nyerere,” amesema
Mfuko wa Udhamini wa Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ulianzishwa Oktoba 12, 2009 ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuenzi mchango wa Baba wa Taifa katika kuendeleza elimu na rasilimali watu nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt.Bill Kiwia amesema, jukumu la kusimamia mchakato wa ufadhili huo ni heshima kubwa kwa taasisi hiyo na ni ishara ya imani iliyowekwa na BoT katika uwezo wa HESLB.
Dkt.Kiwia amesema, ushirikiano huo unaonesha namna taasisi za Serikali zinavyoweza kutumia mifumo na uwezo wao kwa pamoja ili kuboresha huduma kwa Watanzania.
