Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), akijibu maswali bungeni jijini Dodoma, likiwemo swali la Mheshimiwa Haidary Hemed Sumry, Mbunge wa Mpanda mjini aliyetaka kujua mpango wa Serikali kupunguza riba za mikopo ya biashara katika benki ili kuwawezesha wafanyabiashara kulipa mikopo kwa wakati.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha-Dodoma)
Na. John Masele na Martha Mbena, WF – Dodoma.
Serikali imesema inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kisera na kiusimamizi ili kuwezesha benki za biashara kutoa mikopo kwa riba nafuu zaidi ikiwemo kuendelea kutekeleza sera ya fedha inayolenga kudhibiti mfumuko wa bei.
Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mheshimiwa Haidary Hemed Sumry, Mbunge wa Mpanda mjini aliyetaka kujua mpango wa Serikali kupunguza riba za mikopo ya biashara katika benki ili kuwawezesha wafanyabiashara kulipa mikopo kwa wakati.
Mhe. Luswetula alisema kuwa Serikali haiingilii moja kwa moja upangaji wa viwango vya riba za mikopo katika benki za biashara zinazofanya shughuli zake nchini bali huamuliwa kwa kuzingatia misingi ya soko, ikiwamo kiwango cha mfumuko wa bei, vihatarishi vya mikopo kutolipwa, gharama za uendeshaji wa benki husika pamoja na kiwango cha faida wanacholenga kupata.
“Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kisera na kiusimamizi na kuwezesha benki za biashara kutoa mikopo kwa riba nafuu zaidi ikiwemo kuendelea kutekeleza sera ya fedha inayolenga kudhibiti mfumuko wa bei, ambao ni moja ya kiashiria muhimu kinachotumika katika kukokotoa na kuamua riba inayotozwa kwenye mikopo na benki hizi za biashara’’, alifafanua Mhe. Luswetula.
Alisema kuwa katika kufanikisha azma hiyo, Benki Kuu ya Tanzania imeendelea kufanya mabadiliko katika kiwango cha Riba ya Benki Kuu (Central Bank Rate – CBR) kuendana na mwelekeo wa kiuchumi ili kuhakikisha kuwa mfumuko wa bei unabaki ndani ya wigo, huku ikiendelea kuhakikisha uwepo wa kiwango cha kutosha cha ukwasi kwenye uchumi ili kuchagiza upatikanaji wa mikopo kwa gharama nafuu.
Mhe. Luswetula aliongeza kuwa Serikali imeanzisha mfumo wa ulinganishi wa bei unaojulikana kama Price Comparator System unaongeza uwazi kuhusu viwango vya riba na gharama zinazotozwa na taasisi mbalimbali za kifedha, na hivyo kuwasaidia wakopaji kufanya maamuzi sahihi kuhusu huduma za mikopo wanazozihitaji. Vilevile, mfumo huo unachochea ushindani miongoni mwa benki za biashara, jambo linaloweza kuchangia kupungua kwa gharama za mikopo kwa wananchi.
Mhe. Luswetula alisema kuwa hatua nyingine zilizochukuliwa ni pamoja na kuendelea kuhimiza benki na taasisi za fedha kutumia kanzidata ya taarifa za wakopaji (Credit Reference Bureau), ambayo hutoa taarifa za historia ya ukopaji na ulipaji wa madeni ya wakopaji. Mfumo huu hupunguza wasiwasi wa benki kuhusu vihatarishi vya mikopo kutolipwa, hivyo kusaidia kupunguza gharama za tathmini ya mikopo.