Mashindano ya 23 ya Shirikisho la Michezo ya Shule za Sekondari Afrika Mashariki (FEASSA) yamepata msukumo mkubwa baada ya Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB) kutoa udhamini wa Dola za Marekani 90,000, (takribani mil 240) katika kuunga mkono maandalizi na uendeshaji wa mashindano ya shirikisho hilo yanayoendelea mkoani Morogoro.
Mashindano hayo makubwa zaidi ya michezo ya shule katika ukanda wa Afrika Mashariki yamezikutanisha timu 413 na washiriki 5,548 kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki, zinazoshindana katika aina 51 za michezo. Mashindano hayo yanatarajiwa kuhitimishwa Agosti 22, 2026.
Akizungumza katika hafla rasmi ya ufunguzi wa mashindano hayo, Meneja wa EADB nchini Tanzania, Bw. Stephen Wambura, alisema ushirikiano wa Benki hiyo na FEASSA unaakisi dhamira ya EADB ya kuwekeza kwa vijana na kuunga mkono mipango inayochangia maendeleo endelevu katika Afrika Mashariki.
“Ingawa jukumu letu kuu ni kufadhili miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali muhimu za uchumi, tunatambua kuwa maendeleo endelevu hayaishii kwenye miundombinu na shughuli za biashara. Pia yanahusisha kuwawezesha watu, hususan vijana, ambao ndio msingi wa mustakabali wa ukanda wetu,” alisema Bw. Wambura.
Alisema dhamira hiyo ndiyo iliyochochea uamuzi wa EADB kuwa mdhamini mkuu wa Mashindano ya 23 ya FEASSA, kwa kutoa mchango wa Dola za Marekani 90,000 kwa ajili ya kuwezesha mashindano hayo kufanyika kwa mafanikio.
“Udhamini wa michezo ni mojawapo ya nguzo muhimu katika ajenda yetu ya Mipango ya Uwajibikaji wa Kijamii wa Kampuni (CSI), kwa sababu tunaelewa uwezo mkubwa wa michezo katika kujenga tabia, kuhamasisha mtindo bora wa maisha na kufungua fursa kwa vijana katika ukanda wetu,” aliongeza.
“Kupitia udhamini huu, hatuwekezi tu katika mashindano haya, bali pia tunawekeza katika kuwaandaa kizazi kijacho cha viongozi wa Afrika Mashariki.”
Kwa mujibu wa makubaliano ya udhamini, EADB inasaidia utengenezaji wa medali na vikombe kwa ajili ya washindi, pamoja na upatikanaji wa sare za michezo kwa washiriki watakaoshiriki katika hatua za fainali.
Ikiwa mwenyeji wa mashindano ya mwaka huu, Tanzania imetuma moja ya vikosi vikubwa zaidi, ikiwa na timu 127 na washiriki 1,704 wanaoshiriki katika michezo mbalimbali.
Katika mpira wa miguu kwa wavulana, Tanzania inawakilishwa na Shule za Sekondari Nsumba, Mbeya Day, Morogoro na Urambo Day, ambazo zitakuwa na jukumu la kutetea heshima ya nchi katika mashindano hayo.
Kwa upande wa mpira wa miguu kwa wasichana, Tanzania inawakilishwa na Shule za Sekondari Ziba, Fountain Gate na Kilombero, ambazo zinatarajiwa kutumia vyema fursa ya kucheza mbele ya mashabiki wa nyumbani katika kuwania nafasi za juu.
Tanzania pia inalenga kufanya vizuri katika mpira wa wavu. Katika upande wa wavulana, Shule za Sekondari Lumala, Kaliua na Kajunjumele ndizo zinazobeba matumaini ya Tanzania, huku Mengele, Lumala na Mwanhuzi zikiiwakilisha nchi katika mashindano ya wasichana.
Mpira wa kikapu ni miongoni mwa michezo ambayo Tanzania inalenga kutumia vizuri fursa ya kucheza nyumbani. Katika mashindano ya wavulana ya 5×5, Tanzania inawakilishwa na Shule za Sekondari Nsumba, St Jude na Juhudi.
Kwa upande wa wasichana wa 5×5, Shule za Sekondari Orkeeswa, Uru Community na Rungwa ndizo zitakazobeba matumaini ya Tanzania.
Tanzania pia inatarajia kupata matokeo mazuri katika netiboli, mchezo ambao kwa muda mrefu umekuwa miongoni mwa michezo ambayo Tanzania imekuwa ikitoa timu zenye ushindani mkubwa. Shule za Sekondari Mkolani, Vwawa na Mbeya ni miongoni mwa timu zinazotarajiwa kuongoza kinyang’anyiro cha Tanzania katika mchezo huo.
Kwa kuwakutanisha maelfu ya vijana kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki, Michezo ya FEASSA haitoi tu jukwaa la ushindani wa kimichezo, bali pia inawapa vijana fursa ya kukuza vipaji, nidhamu, mshikamano, uwezo wa kufanya kazi kwa pamoja na uongozi, huku ikichangia kuimarisha mshikamano na ushirikiano wa kikanda kupitia michezo.
Kadiri mashindano yanavyoelekea kileleni kuelekea tarehe 22 Agosti, Tanzania inalenga kutumia vyema faida ya kuwa mwenyeji ili kujinyakulia medali katika michezo mbalimbali. Kwa upande wake, udhamini wa EADB unaendelea kusisitiza dhamira ya Benki hiyo ya kuunga mkono mipango inayowekeza katika vijana na kuchangia maendeleo ya muda mrefu ya Afrika Mashariki.

Meneja wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB), Bw. Stephen Wambura (kulia), akikabidhi rasmi sare za michezo kwa Rais wa Shirikisho la Michezo ya Shule za Sekondari Afrika Mashariki (FEASSA), Bw. Justus Mugisha, kwa ajili ya kutumiwa na timu zinazoshiriki katika hatua za fainali za Michezo ya FEASSA zinazoendelea Morogoro, Tanzania. Sare hizo ni sehemu ya udhamini wa Dola za Marekani 90,000 ( takribani mil 240) kutoka EADB kwa ajili ya kufanikisha toleo la 23 la mashindano hayo ya michezo ya shule katika ukanda wa Afrika Mashariki, ambayo yamewakutanisha timu 413 na washiriki 5,548 kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki.