Featured Kitaifa

RAIS DKT. MWINYI: MITANDAO YA KIJAMII IWE JUKWAA LA KUISEMEA SERIKALI NA KUJENGA IMANI YA WANANCHI

Written by Alex Sonna

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewahimiza viongozi na watendaji wakuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutumia mbinu za kisasa katika utoaji wa taarifa na kuimarisha mawasiliano kati ya Serikali na wananchi, ikiwemo kupitia mitandao ya kijamii, huku wakitanguliza wajibu wa kuisemea Serikali na maslahi ya umma badala ya masuala binafsi.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 29 Julai 2026, alipofunga Semina Elekezi kwa Mawaziri, Naibu Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, iliyofanyika kwa siku mbili katika Hoteli ya Golden Tulip Airport, Zanzibar.

Amewataka viongozi hao kutumia kikamilifu vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi katika kutoa ufafanuzi kuhusu sera, mipango na utekelezaji wa Serikali, kuelimisha umma na kukabiliana na upotoshaji, huku wakihakikisha wanajiandaa ipasavyo kabla ya kuzungumza na umma.

Amesema mawasiliano ni nyenzo muhimu ya kujenga uelewa na imani ya wananchi, kuimarisha taswira ya Serikali na kuelekeza mijadala ya umma, hivyo viongozi wanapaswa kuzingatia kwa makini ujumbe wanaoutoa pamoja na mwenendo wao katika majukwaa mbalimbali ya mawasiliano.

Rais Dkt. Mwinyi amesema semina hiyo imeongeza uelewa wa viongozi kuhusu mabadiliko yanayoendelea katika sekta ya mawasiliano Serikalini, yakiwemo maendeleo ya teknolojia, matumizi ya mitandao ya kijamii na akili unde, mabadiliko ya siasa za kimataifa pamoja na mahitaji ya hadhira ya sasa, hususan vijana.

Kuhusu Muungano, amesema semina hiyo imeimarisha uelewa wa viongozi kuhusu misingi na umuhimu wake, huku akiwataka kuendeleza ujumbe unaojenga umoja wa wananchi, kuimarisha ushirikiano baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, pamoja na kuuenzi Muungano kama msingi wa Taifa imara.

Rais Dkt. Mwinyi amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa maono na maelekezo yake ya kufanyika kwa semina hiyo.

About the author

Alex Sonna