Featured Michezo

BMT WAIPONGEZA MONTI INTERNATIONAL KULETA KOCHA BINGWA WA UOGELEAJI,WAITA WATANZANIA KUCHANGAMKIA MAFUNZO

Written by Alex Sonna

 

Mkurugenzi wa Ufundi kutoka Chama cha kuogelea Tanzania, Amina Mfaume (kushoto); Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Shule ya Kimataifa ya Monti, Fatma Fernandes (wa tatu kutoka kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na Kocha mashuhuri wa kimataifa wa uogeleaji, Ben Lee (wa pili kushoto) ambaye aliwasili jijini Dar es Salaam Jumatatu kutokea nchini Marekani kwa lengo la kuendesha kambi ya mafunzo ya uogeleaji kwa wazawa nchini. Mafunzo hayo ya wiki tatu yanaratibiwa na Shule ya Monti. Wengine Ofisa kutoka Baraza la Michezo Tanzania, Petro Gallos (wa pili kutoka kulia).

Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Shule ya Kimataifa ya Monti, Fatma Fernandes (kulia) akiwa na Kocha mashuhuri wa kimataifa wa uogeleaji na mwanzilishi wa RaceBetter, Ben Lee (kushoto) ambaye aliwasili jijini Dar es Salaam Jumatatu kutokea nchini Marekani kwa lengo la kuendesha kambi ya mafunzo ya uogeleaji kwa wazawa nchini. Mafunzo hayo ya wiki tatu yanaratibiwa na Shule ya Kimataifa ya Monti jijini Dar es salaam.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Baraza la Michezo nchini (BMT) limesema ujio wa kocha wa kimataifa wa mchezo wa kuogelea, Ben Lee kutoka Marekani ni fursa kubwa kwa makocha na waogeleaji wazawa kujifunza ujuzi wa viwango vya kimataifa katika mchezo huo hivyo wanapaswa kuhudhuria mafunzo maalumu yatakayotolewa na kocha huyo kwa muda wa wiki tatu.

Kocha Lee, ambaye ana uzoefu mkubwa wa kufundisha waogeleaji katika ngazi za NCAA na Olimpiki, ataongoza programu maalumu ya maendeleo ya uogeleaji katika Shule ya Kimataifa ya Monti jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuboresha viwango vya ushindani wa Tanzania kwenye mashindano ya kimataifa na kuweka msingi wa maendeleo endelevu ya mchezo huo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika mapokezi ya kocha huyo juzi jijini Dar es Salaam, Afisa Michezo wa BMT, Petro Gallos mbali na kupongeza ujio wake, amesema wakufunzi wa ndani wa mchezo huo wanapaswa kutumia mwanya huo adhimu kwa kuchota ujuzi wenye manufaa.

Naye Mkurugenzi wa Ufundi wa Chama cha Uogeleaji Tanzania (TSA), Amina Mfaume alisema; “mafunzo yatakayotolewa na kocha huyo yataongeza ufanisi wa makocha wetu na kutusaidia kuangalia maendeleo ya waogeleaji kwani wale watakaowashiriki wataona jinsi gani makocha wa kimataifa wanavyofanya mafunzo yao.”

Aidha, Mkurugenzi wa Shule ya Kimataifa ya Monti ambao ndio waandaaji wa mafunzo hayo, Fatma Fernandez alisema programu hiyo ni sehemu ya jitihada za kukuza vipaji vya waogeleaji wa Kitanzania na kuijenga Tanzania kuwa kitovu cha maendeleo ya mchezo wa uogeleaji katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Alisema ujio wa Lee umefika katika kipindi muhimu ambacho Tanzania inajiandaa kushiriki mashindano mbalimbali ya kimataifa, yakiwemo Mashindano ya CANA Zone 3, ambapo takribani waogeleaji 40 kutoka nchini wanatarajiwa kuiwakilisha Tanzania.

“Hatutaki tu kuwaandaa waogeleaji kwa mashindano ya sasa, bali tunajenga mfumo wa muda mrefu utakaowezesha Tanzania kuzalisha waogeleaji wenye uwezo wa kushindana kimataifa. Ili kufanikisha hilo ni lazima tuwaimarishe pia makocha na kuwashirikisha wazazi katika safari ya maendeleo ya wanamichezo,” alisema Fernandez.

Alieleza kuwa programu hiyo imegawanywa katika maeneo matatu muhimu yanayowahusu makocha, waogeleaji na wazazi, kwa kuamini kuwa maendeleo ya mwanamichezo yanategemea ushirikiano wa wadau wote.

Kwa mujibu wa ratiba ya programu hiyo, mafunzo kwa makocha yatafanyika kuanzia Julai 28 hadi 30, yakifuatiwa na kambi za mafunzo kwa waogeleaji wa makundi mbalimbali ya umri, huku mafunzo ya juu yakihitimishwa Agosti 14.

Fernandez alisema mafunzo kwa makocha yatatolewa bure kwa makocha wote waliosajiliwa na Chama cha Uogeleaji Tanzania (TSA), licha ya gharama za kumleta kocha huyo wa kimataifa kugharamiwa kikamilifu na Shule ya Kimataifa ya Monti.

Aliongeza kuwa mafunzo hayo yatafanyika katika bwawa la kisasa la kuogelea la Shule ya Kimataifa ya Monti, Mikocheni, kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 5:00 asubuhi kila siku.

Kwa upande wake kocha Ben Lee ambaye pia ni mwanzilishi wa taasisi ya RaceBetter, mbali nakushukuru kwa mapokezi makubwa, alisema ujio wake unalenga kusaidia kuendeleza vipaji vya wazawa kuanzia ngazi za chini na kuweka misingi kwa makocha na waogeleaji kupata mafanikio ya muda mrefu.

About the author

Alex Sonna