Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Taifa Mhe. Othman Masoud Othman wakishuhudia utiaji saini wa ajenda zilizokubaliwa na pande zote mbili kwa ajili ya kufanyiwa kazi baada ya Tamko la Pamoja la Muafaka wa Kisiasa baina ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na ACT-Wazalendo, katika viwanja vya Ikulu Zanzibar tarehe 09 Julai, 2026.
…
Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ametoa wito kwa wananchi wote wa Zanzibar kuunga mkono dhamira njema ya maridhiano baina ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na ACT –Wazalendo, huku akiahidi kuusimamia mchakato huo kwa masilahi ya Zanzibar.
Dk Mwinyi ameyasema hayo leo Julai 9, 2026 mjini Unguja, Zanzibar wakati akishuhudia utiaji saini wa tamko la pamoja la maridhiano ya kisiasa baina ya vyama hivyo, yaliyoanza Novemba 9, 2025.
Amesema hatua ya utiaji saini wa tamko hilo ni hatua muhimu katika kufungua njia kufikia utekelezaji wa matakwa ya kikatiba ya kuwezesha uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kwa mujibu wa kifungu cha 9(3) na 39 vya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
“Natoa wito kwa viongozi wote wa vyama vya siasa na wananchi wote wa Zanzibar kuunga mkono dhamira hii njema ya kuleta maelewano na maridhiano, ili kuchochea maelewano na mustakabali mwema wa nchi yetu.
“Kwa upande wetu viongozi, nawahakikishia wananchi wa Zanzibar kwamba tutausimamia mchakato huu kwa dhamira ya dhati na kuweka mbele masilahi mapana ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla,” amesema Rais Mwinyi.