Featured Kitaifa

‘UTALII NI MBONI YA JICHO LETU’-MTATURU.

Written by mzalendoeditor

MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu ameiomba serikali ijikite katika kulinda rasilimali zilizopo na isiache watu wachache ambao hawana nia njema nan chi wakaharibu vivutio vilivyopo.

Mtaturu ametoa rai hiyo Juni 16,2022,Jijini Dodoma wakati akichangia mapendekezo ya serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2022/2023.

Amesema ni lazima kama nchi iwe na vipaumbele katika kulinda vivutio vilivyopo ili kuenzi kazi nzuri anayoifanya Rais Samia Suluhu Hassan katika kutangaza utalii kupitia filamu ya Tanzania The Royal Tour.

“Utalii ndio unaingiza fedha nyingi kuliko sekta yoyote ,utalii huu tumepewa kama tunu na Mungu, lazima tulinde rasilimiali tulizonazo,na kupitia kazi ya Mh Rais tunaona matokeo yake watu wanakuja nchini,sasa leo hii tukitangaza vivutio ambavyo kesho havipo inakuwa haina maana,

“Niombe sana serikali isiache watu wachache ambao hawana nia njema waharibu vivutio vyetu,wengine wanakuja na sababu ndogo tu kuwa serikali inawajali wanyama kuliko wananchi hii sio kweli,wote wanaishi nchi hii ila lazima tuwe na vipaumbele tulinde vivutio na huku tunalinda na binadamu hatuwezi kuruhusu hali hii eti kwa sababu kuna watu wataona wanaonewa,”ameongeza.

Amesema pori la Loliondo lilianzishwa mwaka 1951 na kama lingekuwa halijahifadhiwa leo hii kungekuwa hakuna vivutio.

“Hatuwezi kuacha watu wachache wakatuharibia tena bahati mbaya wanatumika nan chi nyingine kuharibifu kwa sababu ya ushindani wa utalii,niombe serikali iwe makini vinginevyo tutaanza kuingia kwenye huruma ambazo hazina sababu ,wengine wana ajenda zao,”amesema.

Amesema pori hilo lilikuwa na mita za mraba 4,000, serikali imepunguza mita za mraba 2,500 na kuwaachia wananchi wafanye shughuli zao na eneo la mita za mraba 1,500 ni chanzo cha ikolojia ya kulinda Serengeti.

“Leo Serengeti ni mbuga inayosifika duniani, watu wengi wanataka kuja kuiangalia Serengeti,pale kuna Nyumbu wanapita kila mwaka na kuzaliana ,vyanzo vya maji ambavyo vinapatikana kutunza Serengeti vinapitia pale Loliondo,sasa tukianza kuja na sababu ndogo ndogo haina mashiko,

“Tanzani bado ni kubwa,ardhi hii ipo chini ya Rais aruhusu waende popote wakaishi waache eneo hilo liweze kulindwa na kuhifadhiwa ili tuweze kuendelea kupata watalii kama ambavyo tumeendelea kulinda katika miaka yote tangu mwaka 1951,”amebainisha.

Mtaturu amesema sekta ya utalii imeendelea kuonekana kama mboni ya jicho hivyo serikali isisite kuchukua hatua na kusimamia.

‘Naomba sana kama kuna mtu anafanya tofauti na haki za binadamu wachukuliwe kuwa ni wao lakini sio ionekane serikali nzima haijafanya kazi yake,”amesema.

About the author

mzalendoeditor