Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Aprili 30,2026 bungeni Dodoma.
Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeliomba Bunge kuidhinisha jumla ya shilingi bilioni 222.59 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu na vipaumbele vyake katika mwaka wa fedha 2026/2027.
Akiwasilisha makadirio hayo bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, amesema mkazo mkubwa umewekwa kwenye miradi ya maendeleo ili kuharakisha mageuzi ya kidijitali nchini.
Kwa mujibu wa mgawanyo huo, shilingi bilioni 13.15 sawa na asilimia 5.9 zimetengwa kwa matumizi ya kawaida, ambapo shilingi bilioni 6.37 ni mishahara ya watumishi na shilingi bilioni 6.77 ni matumizi mengineyo.
Kwa upande wa maendeleo, wizara imepanga kutumia shilingi bilioni 209.44, sawa na asilimia 94.1 ya bajeti yote.
Aidha, kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 98.48 ni fedha za ndani huku shilingi bilioni 110.96 zikiwa ni fedha za nje, hatua inayoonyesha kuendelea kwa ushirikiano wa kimataifa katika kukuza sekta ya TEHAMA.