Featured Kitaifa

NEMC KANDA YA KASKAZINI YASISITIZA KUWA NA MFUMO WA KUTENGANISHA TAKA ILI KUTUNZA NA KUHIFADHI MAZINGIRA.

Written by mzalendoeditor

Meneja wa baraza la taifa la hifadhi na usimamizi wa mazingira (NEMC) Kanda ya Kaskazini  Lewis Nzali akiongea katika maadhimisho ya siku ya mazingira yaliyofanyika kikanda mkoa Arusha.

Mkuu wa kitengo cha mazingira  kutoka bodi ya maji  ya Bonde la mto Pangani  Mhandisi Arafa Magidi  akiongea katika maadhimisho ya siku ya mazingira.

Lucas Kaaya diwani wa Kata ya King’ori na Mwenyekiti wa kamati ya uchumi ,ujenzi na mazingira akiongea katika maadhimisho ya siku ya mazingira.

Picha ya pamoja  ya wadau wa mazingira katika maadhimisho ya siku ya mazingira duniania yaliyofanyika kikanda mkoa wa Arusha

………………………………………….
NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA 
Baraza la taifa la hifadhi na usimamizi wa mazingira(NEMC) Kanda ya Kaskazini limesisitiza kuwa na mfumo wa kutenganisha taka  za plastic, vyakula na taka nyingine ili kuweza kutunza na kuhifadhi mazingira pamoja na kutumia taka kama fursa badala ya kero.
Hayo yamesemwa na meneja wa NEMC Kanda ya Kaskazini Lewis Nzali katika kongamano la kuadhimisha siku ya mazingira duniania iliyofanyika kikanda katika halmashauri ya Meru mkoani Arusha ambapo alisema kuwa kwa kuweka mfumo huo itasaidia utunzaji wa mazingira kwani itakuwa ni rahisi kurudisha taka za plastic katika soko na taka za chakula kuzalisha mbolea .
Alisema kuwa ni vema wananchi wakawa na vyombo tofauti  kila taka ikawekwasehemu yake na kutolea mfano mabaki ya chakula kutengenezewa mboji ambapo katika maeneo mengine yaliyopiga atua zaidi mabaki hayo kama vile maganda ya ndizi na mapapa  yanatengenezewa Gesi asilia.
“Taka ni fursa na sio kero kinachotakiwa ni kujua unatumiaje  na taka za plastic kama vile mifuko na chupa hivyo vinaweza vikarejelezwa na kwahati nzuri tuna kampuni mbalimbali hapa Arusha ambazo zimeanza kurejeleza kwa kutengeneza vitu vingine kama mabenchi, viti, meza pamoja na nguzo ambazo zinaweza zikatumika kwaajili ya uzio kwasababu vinachukua muda mrefu haviliwi na mchwa wala haviozi kirahisi,” Alifafanua.
“Ni vema watu watatumia fursa hiyo ya mazingira kwa kuhakikisha kuwa wanatenga taka kwaajili ya manufaa zaidi ikiwemo kurahisisha urejelezaji badala ya kuweka sehemu muja ukazalisha Nzi na kuweza kuleta magonjwa mengine kama vile tumbo kwani asilimia 40 ya magonjwa yanayotukabili yansababishwa na uchafuzi wa mazingira,”Alieleza.
Alisema Nzi wanasambaza magonjwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine  lakini kama uchafu  utakuwa umedhibitiwa kwa kutengeneza mboji hawataweza kuzaana kwasababu hawana chakula hivyo watapungua na magonjwa yanayosambazwa na Nzi pia yatapungua.
Kwa upande wake  Lucas  Kaaya diwani wa Kata ya King’ori na  Mwenyekiti wa kamati ya uchumi ,ujenzi na mazingira ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alitoa rai  kwa jamii, kila mmoja kutambua kuwa yeye ni mdau wa mazingira na anawajibu wa kuhakikisha mazingira yanakuwa salama muda wote kwani hakuna maisha bila mazingira salama.
“Mazingira yaliyohifadhiwa ndio uchumi wa taifa, nitoe wito kwa watendaji wa serikali na wananchi kutimiza wajibu wao kutunza mazingira kwa kutii sheria za mazingira na kutoharibu ikolojia,” Alisema.
Nao wadau wa mazingira walitoa elimu juu ya umuhimu wa kutunza mazingira pamoja na madhara ya plastic ambapo Erick Kato  mtafiti kutoka Taasisi ya Nelson Mandela  alisema mbali na jitihada za serikali kudhibiti madhara ya matumizi ya plastic kwa kupiga marufuku matumizi ya mifuko,  bado nguvu  zaidi inahitajika katika kudhibiti matumizi ya plastiki inayoleta madhara ardhini, kwa wanyama ,binadamu na hewa kwa ujumla.
“Madhara ya plastic ndogondogo (microplastics) kwa Binadamu   ni pamoja na kuathiri mfumo wa uzazi na hewa ambapo amebainisha  plastiki huingia kwa binadamu kupitia kwenye vyakula vya moto vinavyowekwa lenye vyombo vya plastic au mifuko,” Alisema.
 Mkuu wa kitengo cha mazingira  kutoka bodi ya Bonde la mto Pangani  Mhandisi Arafa Magidi alisema ni vema jamii ikaishi kwenye Kauli mbiu ya mwaka huu  ya siku ya Mazingira duniani ya “Tanzania ni moja tu,tunza Mazingira ” ambapo amebainisha  watanzania wanapaswa kutunza vyanzo vya maji vilivyopo tanzania kwani hakuna namna ya kuchukua vyanzo  kwenye sayari nyingine.

About the author

mzalendoeditor