Featured Kitaifa

WATENDAJI WA UCHAGUZI WATAKIWA KUEPUKA KUFANYA KAZI KWA MAZOEA

Written by Alex Sonna

 

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele akizungumza Mkoani Morogoro leo tarehe 28 Aprili, 2026 wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa  watendaji wa uchaguzi.

Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Kisheria wa Tume, Ndg. Cyprian Mbugano akiwasilisha mada kuhusu majukumu ya Watendaji wa Uchaguzi na mambo muhimu ya kuzingatia. 

Sehemu ya washiriki ambao ni watendaji wa Uchaguzi kutoka katika Jimbo la Isimani na Kata 12 za Tanzania Bara wakifuatilia hotuba ya ufunguzi.

Sehemu ya washiriki ambao ni watendaji wa Uchaguzi kutoka katika Jimbo la Isimani na Kata 12 za Tanzania Bara wakifuatilia hotuba ya ufunguzi.

Mkurugenziu wa Ofisi ya Zanzibar, Ndg. Adam Mkina akiwasilisha mada 

Meza Kuu ikiwa katika ukumbi wa mafunzo

 

Sehemu ya washiriki ambao ni watendaji wa Uchaguzi kutoka katika Jimbo la Isimani na Kata 12 za Tanzania Bara wakifuatilia hotuba ya ufunguzi.

Waratibu wa Uchaguzi wa Mikoa, Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi Ngazi ya Jimbo, Wasimamizi wa Uchaguzi Ngazi ya Kata, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ununuzi na Wahasibu wakila viapo vya kujitoa uanachama chama cha siasa na kile cha kutunza siri.

 

Waratibu wa Uchaguzi wa Mikoa, Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi Ngazi ya Jimbo, Wasimamizi wa Uchaguzi Ngazi ya Kata, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ununuzi na Wahasibu wakila viapo vya kujitoa uanachama chama cha siasa na kile cha kutunza siri.

****************

Na. Mwandishi Wetu, Morogoro

Watendaji wa uchaguzi
wametakiwa kuepuka kufanya kazi kwa mazoea licha ya baadhi yao kuwa na uzoefu
kwenye masuala ya uchaguzi.


Wito huo umetolewa na Mwenyekiti
wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs
Mwambegele leo tarehe 28 Aprili, 2026 mkoani Morogoro wakati akifungua mafunzo
ya watendaji wa uchaguzi.

Mafunzo hayo ni sehemu ya
mchakato wa maandalizi ya uchaguzi mdogo wa ubunge kwenye Jimbo la Ismani
Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Mkoani Iringa na Kata 12 za Tanzania Bara unaotarajiwa
kufanyika tarehe 01 Juni, 2026.

“Nachukua nafasi hii kuwaasa
kuwa, pamoja na uzoefu ambao baadhi yenu mnao katika uendeshaji wa uchaguzi,
mhakikishe mnazingatia maelekezo mtakayopewa na Tume badala ya kufanya kazi kwa
mazoea. Kwani kila uchaguzi unatofautiana na uchaguzi mwingine,” amesema Jaji
Mwambegele.

Ameongeza
kuwa watendaji hao wa uchaguzi wanapaswa kuzingatia sheria, kanuni na maelekezo
watakayopewa na Tume ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba wanavishirikisha
vyama vya siasa katika hatua zote kuelekea uchaguzi huo.  

 “Wakati wote wa mchakato wa uchaguzi huu, ni
vema mkavishirikisha kwa karibu vyama vyote vya siasa vyenye usajili kamili na
wadau wengine wa uchaguzi katika maeneo yenu kuhusu masuala ya kiuchaguzi
ambayo wanastahili kushirikishwa kwani jambo hilo litawarahisishia utekelezaji
wa majukumu yenu,” amesema Jaji Mwambegele.

Amewataka watendaji hao kufanya
utambuzi wa vituo vya kupigia kura mapema ili kubaini mahitaji maalum ya vituo
husika na kuhakikisha kunakuwa na mpangilio mzuri ambao utaruhusu uchaguzi
kufanyika kwa utulivu na amani.

Jaji Mwambegele
amewasisitiza watendaji hao kuhakikisha wanaajiri watendaji wa vituo wenye sifa,
weledi, wanaojitambua na kuachana na upendeleo kwa ndugu na jamaa ambao hawana
sifa za kufanya shughuli za uchaguzi.

“Mhakiki vifaa vya uchaguzi
mnavyopokea kutoka Tume na kuhakikisha kila mkuu wa kituo anapata vifaa vyote
vya uchaguzi vinavyohitajika mapema na muweke utaratibu utakaowezesha kila
kituo cha kupigia kura kufunguliwa saa 1:00 asubuhi,” amesema.

Mafunzo hayo ya siku tatu
yamewahusisha Waratibu wa Uchaguzi wa Mikoa, Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi
Wasaidizi wa Uchaguzi Ngazi ya Jimbo, Wasimamizi wa Uchaguzi Ngazi ya Kata,
Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ununuzi na Wahasibu.

Kata 12 za Tanzania Bara
zitakazofanya uchaguzi wa Udiwani ni Mzimuni iliyopo Manispaa ya Kinondoni;
Zongomera, Manispaa ya Kahama; Itilo, Halmashauri ya Mji wa Nzega; Ketare,
Halmashauri ya Mji wa Tarime na
Nyumbigwa,
Halmashauri ya Mji wa Kasulu.

Nyingine
ni kata ya Kala iliyoko Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi; Ziba, Halmashauri ya
Wilaya Igunga; Kamsisi, Halmashauri ya Wilaya ya Mlele; Nyamugali, Halmashauri
ya wilaya ya Buhigwe; Namasakata Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru; Bwongera, Halmashauri
ya Wilaya ya Chato na Kibiti Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti.

About the author

Alex Sonna