Featured Kitaifa

OFISI YA RAIS,MIPANGO NA UWEKEZAJI YAOMBA BILIONI 144.85 BAJETI YA MWAKA 2026/27

Written by Alex Sonna

Waziri Wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027.

Dodoma

Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji imewasilisha rasmi bungeni ombi la kuidhinisha jumla ya shilingi Bilioni 144.85 kwa ajili ya mwaka wa fedha 2026/27, fedha zitakazogharamia matumizi ya kawaida pamoja na miradi ya maendeleo.

Waziri Wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo,ameyasema hayo bungeni Dodoma wakati  akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027.

Akiwasilisha hotuba hiyo bungeni  Waziri Mkumbo, amesema kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 126.01 zimetengwa kwa matumizi ya kawaida huku shilingi bilioni 18.83 zikielekezwa kwenye miradi ya maendeleo.

Ameeleza kuwa lengo kuu la bajeti hiyo ni kuhakikisha taasisi zilizo chini ya ofisi hiyo zinaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, huku pia zikichochea ukuaji wa uchumi kupitia uwekezaji na mipango madhubuti ya maendeleo.

Kwa mujibu wa uchambuzi wa mafungu mbalimbali, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji (Fungu 011) imetengewa jumla ya shilingi bilioni 35.38, ambapo kati ya hizo, bilioni 26.24 ni kwa matumizi ya kawaida na bilioni 9.14 kwa miradi ya maendeleo.

Aidha, Tume ya Taifa ya Mipango (Fungu 066) imepangiwa kutumia shilingi bilioni 48.64, ikiwa ni pamoja na bilioni 39.32 kwa matumizi ya kawaida na bilioni 9.31 kwa miradi ya maendeleo.

Kwa upande wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (Fungu 07), jumla ya shilingi bilioni 60.82 zimetengwa, ambapo kiasi kikubwa cha bilioni 60.45 ni kwa matumizi ya kawaida na bilioni 0.37 kwa miradi ya maendeleo.

Waziri huyo alisisitiza kuwa mgao huo umezingatia vipaumbele vya taifa ikiwa ni pamoja na kuimarisha mifumo ya uwekezaji, usimamizi wa rasilimali za umma pamoja na kupanga kwa ufanisi maendeleo ya muda mrefu.

Hata hivyo, baadhi ya wabunge walieleza haja ya kuongezwa kwa fedha za miradi ya maendeleo ili kuhakikisha matokeo chanya yanaonekana kwa wananchi, hususan katika sekta zinazogusa maisha ya moja kwa moja.

Mjadalani kuhusu bajeti hiyo unatarajiwa kuendelea bungeni kwa siku kadhaa kabla ya kufikia hatua ya kupigiwa kura ili kuidhinishwa rasmi.

About the author

Alex Sonna