Naibu Katibu Mkuu Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu,Prof Daniel Mushi,akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau wa TESP na kuhitimisha mradi huo uliofanyika leo Aprili 9,2026 jijini Dodoma kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo.
Na.Alex Sonna-Mzalendo blog-DODOMA
SERIKALI imesisitiza umuhimu wa kuendeleza mafanikio yaliyopatikana kupitia Mradi wa Kusaidia Elimu ya Ualimu (TESP), ili kuhakikisha ubora wa elimu unaimarika kwa vizazi vijavyo.
Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu,Prof Daniel Mushi, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau wa TESP na kuhitimisha mradi huo uliofanyika leo Aprili 9,2026 jijini Dodoma kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Ualimu Tabora, Bi. Balbina Joseph, amesema kuwa Mradi wa Kuendeleza Elimu ya Ualimu (Teachers Education Support Program – TESP), umeleta maboresho makubwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo utunzaji wa mazingira, usawa wa kijinsia, ujumuishi na upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia. Ameongeza kuwa wakufunzi, watumishi na bodi za vyuo wamepata mafunzo yaliyoongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Naye Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ualimu Kabanga, Bw. Phonce Mashibe, amesema chuo hicho kimenufaika kwa kiasi kikubwa kupitia ujenzi upya wa miundombinu na uwekezaji katika mifumo ya nishati mbadala. Amefafanua kuwa matumizi ya biogas na nishati ya jua yamepunguza gharama za uendeshaji kwa kiasi kikubwa, zikishuka hadi asilimia 60.
Kwa upande wa wanafunzi, Marry Faustine Igulu, mwanafunzi wa Chuo cha Ualimu Bustani ngazi ya diploma, amesema kuwa Mradi wa Kuendeleza Elimu ya Ualimu (Teachers Education Support Program – TESP),umeboresha kwa kiwango kikubwa mazingira ya kujifunzia, ikiwemo ujenzi wa maabara za sayansi, ukarabati wa mabweni, madarasa na maktaba. Ameongeza kuwa upatikanaji wa vifaa vya TEHAMA umeongeza uwezo wa walimu tarajali kutumia teknolojia katika ufundishaji, hatua inayochangia kuinua ubora wa elimu nchini.
