Serikali ya Uswisi inatarajia kutoa zaidi ya bilioni 20 kwa ajili ya kuendelea kuimarisha maeneo ujuzi, ajira pamoja na vyuo vya ufundi nchini.
Hayo yamebainishwa leo jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Uswisi nchini Mhe. Didier Chassot.
Katika mazungumzo hayo Prof. Mkenda amemshukuru Balozi huyo kwa ufadhili wa miradi mbalimbali ya Elimu ikiwemo eneo la ufundi na ujuzi ambapo amesema ajenda kubwa kwa sasa katika Sekta ya Elimu ni mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 na mabadiliko ya mitaala.
“Mapitio ya Sera na mabadiliko ya Mitaala inalenga kuhakikisha elimu yetu kuwa na uwezo wa kumjenga mhitimu kuwa na ujuzi wa kutosha wa kuingia katika soko la ajira kwa kujiajiri ama kuajiriwa bila kuathiri ubora wa elimu,” amesema Prof. Mkenda.
Prof. Mkenda ameongeza kuwa moja ya eneo ambalo Uswisi wako vizuri ni upande wa ukarimu na utalii ambapo amemuomba Balozi huyo kuona namna ambavyo nchi hizi mbili zinaweza kuwa na mpango wa pamoja wa kubadilisha wataalamu hasa Wakufunzi kutoka katika Vyuo vya Ufundi nchini ili kuwawezesha kupata ujuzi wa jinsi ya kufundisha vijana wa Kitanzania katika eneo hilo.
Akizungumzia Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, Waziri Mkenda amesema kuwa kwa kiwango kikubwa Sera hiyo inajibu hoja ambazo watu wengi wamekuwa wakitaka kuziona kwenye elimu, hivyo mapitio hayo yatawezesha nchi kuamua kwa pamoja kama sera hiyo itekelezwe na kwa namna gani kwa kuwa utekelezaji wake unahitaji uwekezaji wa nyongeza katika Elimu.
“Tayari tumeshapokea maoni mengi kutoka kwa wadau wa elimu ambapo yanafanyiwa kazi na hivi karibuni tutakuwa na mkutano mwingine wa kuendelea kupokea maoni ili ifikapo mwishoni mwa mwaka tuwe na rasimu ya sera na mitaala ambayo imependekezwa na wadau,” amesema Prof. Mkenda.
Kwa upande wake Balozi wa Uswisi nchini Mhe. Didier Chassot amesema Serikali ya Uswisi itaendelea kuisaidia Tanzania katika kuimarisha taasisi zinazotoa mafunzo ya ufundi nchini ili ujuzi unaohitajika kumsaidia kijana kuingia katika soko la ajira upatikane pamoja na kuchangia katika jitihada za mageuzi ya elimu.