Featured Kitaifa

KIKUNDI CHA AMANI NCHINI WAFANYA MKUTANO MAALUMU ULIOLENGA KUHAMASISHA UZALENDO NA KUELEZEA MAFANIKIO YA SERIKALI

Written by Alex Sonna

Na Oscar Assenga,Tanga

KIKUNDI cha Amani nchini kimefanya mkutano maalumu leo katika Jiji la Tanga  uliolenga kuhamasisha uzalendo, kuelezea mafanikio ya Serikali na kupongeza utekelezaji wa ahadi za siku 100 za Rais tangu alipochaguliwa 2025.

Akizungumza wakati wa mkutano huo Maalumu Mwenyekiti wa Kikundi hicho nchini Hassan Kubebelwa alitoa wito kwa watanzania hususani vijana wametakiwa kuwa wazalendo kwa nchi na kuacha kukubali
kushawishiwa na watu wanaoshinda kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii kueleza
mabaya pekee na kuficha mazuri mengi yanayofanywa na Serikali

Katika kulitilia mkazo jambo hilo aliiomba Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
(TCRA) na Jeshi la Polisi, kuongeza kasi ya kuwafuatilia na kuwachukulia hatua
kali watu wanaojiita wanaharakati wa mitandaoni wanaotumia majukwaa hayo
kupotosha ukweli na kuichafua Serikali

“Lengo la kuja Tanga ni kuwahamasisha wanakikundi wenzetu wasimame
kidete kuelezea maendeleo ya miundombinu mkoani hapa na nchi nzima. Tuache
kusikiliza upotoshaji wa mitandaoni; Serikali imaleta fedha za mikopo ya
asilimia 10 kwenye halmashauri, watu wakope na kujiendeleza badala ya
kulalamika,” alisisitiza Kubebelwa.

Awali akisoma riskala ya kikundi hicho, Mjumbe wa Kikundi hicho, Rehema
Manyama alieleza katika kipindi cha siku 100, Rais ameonyesha dira kwa
kufanikisha utoaji wa Bima ya Afya kwa wote, kuzalisha ajira kwa vijana ikiwemo
kutoa mikopo.

Aidha alitoa ushauri wake kwa ngazi za mikoa ziendelee kutoa elimu ya
uzalendo na kuimarisha elimu ya amali ili vijana wajiajiri na kuingiza kipato

 

Naye Mjumbe Zuberi Gogo, alibainisha kuwa ingawa hitilafu ndogo ndogo
haziwezi kukosekana, changamoto kubwa inatokana na baadhi ya watendaji wanaopindisha
taratibu na kuigombanisha Serikali na wananchi. Alitoa wito kwa wananchi
kuelewa taratibu za kiserikali ili wasipotezwe na upotoshaji.

Akizungumzia suala la mikopo, Mjumbe Zainabu Salim Ugata, alifafanua
kuwa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri haina upendeleo, bali
inatolewa kwa vikundi vilivyofuata taratibu zote zilizowekwa. Alisema kikundi
hicho kitaendelea kuzunguka mikoa yote nchini kutoa elimu kwa umma ili kuongeza
uelewa wa mambo ya Serikali.

Washiriki wa mkutano huo waliazimia kuwa ni wajibu wa kila mzalendo
kuilinda taswira ya nchi na kuhakikisha kuwa fursa za kiuchumi zinazotolewa na
Rais zinawafikia walengwa bila vikwazo.

 

About the author

Alex Sonna