Katibu Mkuu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Fred Msemwa, akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 1,2026 jijini Dodoma kuhusu Maandalizi ya kuanza kwa utekelezaji wa Dira 2050.
Na.Alex Sonna-DODOMA
TUME ya Taifa ya Mipango (NPC) inatarajiwa kuwasilisha kesho Februari 2,2026 Bungeni Dodoma nyenzo tatu kuu za utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ili kuwapa wabunge fursa ya kujadili na kufanya maamuzi kuhusu utekelezaji wa Dira hiyo pamoja na mipango ya maendeleo ya nchi.
Hayo yamesemwa leo Februari 1,2026 jijini Dodoma na Katibu Mkuu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Fred Msemwa, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Maandalizi ya kuanza kwa utekelezaji wa Dira 2050.
Dkt. Msemwa amesema nyenzo hizo zimeandaliwa na kujadiliwa kwa mujibu wa sheria na zimepitia ngazi zote za maamuzi serikalini kabla ya kuwasilishwa Bungeni.
Amezitaja nyenzo hizo tatu kuwa ni Mpango Elekezi wa Muda Mrefu wa miaka 25 kuanzia mwaka 2026/2027 hadi 2050/2051, Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, pamoja na mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2026/2027.
Amesema baada ya kuwasilishwa Bungeni, wabunge watazijadili na baadaye Bunge kufanya maamuzi ya namna ya utekelezaji wa mipango hiyo ya kimkakati kwa maendeleo ya taifa.
Aidha, Dkt. Msemwa amesema Tume ya Taifa ya Mipango imeandaa nyenzo nyingine za ziada zitakazosaidia kuhakikisha Mamlaka za Serikali za Mitaa ikiwemo miji, manispaa, mikoa, pamoja na taasisi za umma, wizara na idara mbalimbali zinaelewa na kutafsiri kwa usahihi matarajio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Kwa msingi huo, NPC imeandaa Mwongozo wa Upangaji wa Mipango ya Taifa ili kuwe na uelewa wa pamoja miongoni mwa wadau. Tayari tumeendesha semina kwa viongozi kutoka halmashauri, idara, miji na taasisi za umma ili kujadili mwongozo huo,” amesema Dkt. Msemwa.
Kwa mujibu wa Dkt.Msemwa, Tume ya Taifa ya Mipango ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha mfumo wa kielektroniki wa ufuatiliaji na tathmini unaolenga kuleta mageuzi katika ufuatiliaji wa utekelezaji wa mipango kwa kuzingatia zaidi matokeo na uwajibikaji. Mfumo huo unatarajiwa kuanza kutumika sambamba na utekelezaji wa Dira ya 2050 kuanzia Julai 2026.
Hata hivyo ametoa wito kwa wananchi na wadau wote kufuatilia kwa karibu uwasilishaji wa Mpango Elekezi wa Muda Mrefu wa 2026/2027–2050/2051, Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031, pamoja na mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa 2026/2027, utakaowasilishwa Bungeni na Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo.
Amesema ni muhimu kwa wananchi kufuatilia hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya utekelezaji wa Dira hiyo kwa kuwa imebeba matumaini ya taifa, imezingatia maoni ya wananchi na ni fursa ya kipekee kwa kila Mtanzania, kwani uwasilishaji wa mipango ya aina hiyo hufanyika mara chache.
Aidha, Dkt. Msemwa amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inasisitiza ustawi wa pamoja na ushiriki wa kila mwananchi katika ujenzi wa taifa.
“Dira ya 2050 ni alama ya umoja wetu na nia yetu thabiti ya kutomwacha Mtanzania hata mmoja nyuma. Hivyo ni muhimu kwa kila Mtanzania kuwa na taarifa kamili kuhusu kinachoendelea katika mipango ya taifa,” amesisitiza.